2018-02-24 08:50:00

Papa Francisko anatembelea Parokia ya Mt. Gelasio, Jimbo kuu la Roma


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima inakazia umuhimu wa imani inayomwilishwa katika matendo mema. Kristo Yesu ndiye utimilifu wa Sheria na Manabii kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake unaoshuhudia utukufu wa Mwana mpendwa wa Mungu! Yesu aliwaandaa wafuasi wake ili kuweza kukabiliana na Fumbo la Msalaba kwa imani na matumaini zaidi kwa kung’ara uso mbele ya wafuasi wake. Katika maadhimisho haya, Jumapili tarehe 25 Februari 2018, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutembelea Parokia ya Mtakatifu “Gelasio” iliyoko Kaskazini mwa Jimbo kuu la Roma.

Hii itakuwa ni nafasi kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na vijana; wagonjwa, familia pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Parokiani hapo, Caritas. Kama mchungaji, ataadhimisha Sakramenti ya Upatanisho kwa waamini watakaokuwa wamejiandaa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, tayari kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, majira ya jioni! Jumuiya ya Parokia ya Mtakatifu “Gelasio” imekuwa na maandalizi ya maisha ya kiroho, ili kuweza kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao!

Parokia hii ilianzishwa kunako mwaka 1972 na tangu wakati huo imekuwa moto moto katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa kujikita katika katekesi makini kwa watoto wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa, Utume kwa vijana na familia. Parokia hii ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, kwani inatoa huduma kwa maskini na wahitaji. Parokia pia imeanzisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinazokutana ili kusali, kutafakari na kufanya matendo ya huruma. Kati ya viongozi wanaotarajiwa kumkaribisha Baba Mtakatifu Parokiani hapo ni pamoja na Askofu mkuu Angelo De Donatis, Askofu msaidizi Guerino Di Tora, Paroko Giuesseppe Raciti, Paroko usu Alfio Carbonaro pamoja na mapadre wengine kama Miguel Porres Prieto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.