2018-02-23 15:10:00

Kanisa liwe ni chombo cha uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda!


Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Ni muhtasari wa kiu na matamanio halali ya binadamu: kiroho na kimwili, kimsingi hizi ni “Heri za Kiu”, sheria inayogusa undani wa maisha ya binadamu, kiini cha maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani; mchungaji mwema aliyethubutu kuwaacha kondoo wengine wote na kuanza kumtafuta kondoo aliyepotea. Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; upendo uliomwilishwa katika Fumbo la Umwilisho na kupata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Kumbe, Wakristo wanapaswa kuiga mfano wa maisha na utume wa Kristo kwa kumwilisha “Heri za Kiu” katika vipaumbele vyao, kwani, heri hizi ni chemchemi ya wokovu na maisha mapya yanayofumbatwa katika upendo na imani kwa wale wote wanaozipokea kama ilivyokuwa kwa Zakayo Mtoza ushuru aliyejitaabisha kukutana na Kristo Yesu katika maisha yake! Akawekeza katika imani, akavuna upendo, maisha mapya, huruma na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakuna mwamini yeyote anayeweza kujigamba kwamba, ametosheka na kuzima kiu ya maisha yake ya kiroho, kwani hizi ni chachu ya mapambano ya maisha ya kiroho.  

Jamii inawahitaji mashuhuda na vyombo vya amani inayomwilishwa kila siku katika uhalisia wa maisha ya watu! Hawa ni watu wenye uwepo wa kupenda na kupendwa; kutangaza na kushuhudia ukweli kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama Hospitali iliyoko kwenye uwanja wa mapambano, tayari kuganga na kuponya majeraha ya wati wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha. Kanisa linahamasishwa kuonesha ari na moyo wa kimisionari ili kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na huduma kwa maskini, ili hata wao waweze kushiriki katika karamu ya mwanakondoo.

Kanisa halina budi kuendelea kujipyaisha daima katika sera, mikakati na mipango yake ya shughuli za kichungaji kwa kusoma alama za nyakati, ili kuzima kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha ya watu! Wakristo wanapaswa kuwa ni Jumuiya  ambayo ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa watu wa Mataifa. Iwe ni mahali panapowakutanisha watu ili kujibu kilio chao cha ndani: kiroho na kimwili; kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; huruma, upendo na mshikamano wa huduma makini! Mang’amuzi ya kiu ya imani, yawasaidie waamini kujikita katika tafiti moyo ili kutambua kiu na matamanio yao ya kumwona Mwenyezi Mungu.

Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanajipatanisha na kiu yao kwa kutambua kwamba, kiu yao ni kiini cha heri maishani! Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Ijumaa, tarehe 23 Februari 2018 huko Ariccia, nje kidogo ya Roma, kabla ya kufunga mafungo haya ili kumwezesha Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake waandamizi, kurejea tena katika maisha na utume wao wa kawaida.

Padre Josè Tolentino de Mendonca anaendelea kufafanua kwamba, Bikira Maria, kielelezo na mfano wa Kanisa linalosafiri hapa duniani, katika utenzi wake “Magnificat” anakiri kwamba, kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa na chimbuko la heri hii ni Fumbo la Umwilisho pamoja na hija nzima ya maisha ya Bikira Maria hadi pale alipodiriki kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya mwanaye mpendwa.

Bikira Maria ni chemchemi ya maisha yanayopeleka watu kwenye uzima wa milele. Ni mfano bora wa kuigwa wa majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na mja wake; majadiliano yanayosimikwa katika mshangao na mahangaiko ya ndani lakini anafarijiwa kwa kuambia kwamba, Maria usiogope! Naye akajiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili atende kama anavyotaka. Bikira Maria ni mama aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kusikiliza kwa makini; mwamini na mkweli katika maisha na kwamba, ni mama wa huduma makini kwa jirani zake. Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, linakuwa ni chombo cha huduma, ili kuzima kiu na mahangaiko ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Padre Josè Tolentino de Mendonca anakumbusha kwamba, akina mama wamepewa dhamana ya kuwa ni watu wa kwanza wanaopaswa kuzima kiu na njaa ya watoto wao katika medani mbali mbali za maisha dhamana ambayo kamwe haina mbadala. Bikira Maria ni kielelezo makini cha umama wa Kanisa, vinginevyo, Kanisa litakuwa ni mkusanyiko wa watu! Kanisa halina budi kuwa ni alama na shuhuda wa upendo, huruma, imani na matumaini. Bikira Maria ni nyota ya unjilishaji mpya, aendelee kulichangamotisha Kanisa ili liwe kweli chombo cha uinjilishaji mpya. Huu ndio wakati wa kutekeleza haya yote katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.