2018-02-22 10:43:00

Jifunzeni kumwilisha Injili ya Huruma ya Mungu katika maisha!


Mfano wa Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu unasimulia mahusiano katika familia ya binadamu, furaha, changamoto na huzuni zake, kila mtu kadiri ya jangwa la maisha yake, lakini jambo la msingi linalowaunganisha wote ni uhuru ambao wakati mwingine unasigana kimsingi na sheria, kanuni na taratibu za maisha. Mwana mpotevu ni kielelezo cha uhuru usiokuwa na mipaka, uhuru unaomtumbukiza mtu katika majanga ya maisha kiasi cha kujisikia kuwa mtupu na mpweke. Kijana mkubwa licha ya kuwa karibu sana na Baba yake lakini alikuwa na matamanio mabaya, kiasi cha kushindwa kuishi umoja, upendo na udugu na kamwe hakuwa hata na chembe ya huruma na msamaha.

Huu ndio ukweli wa maisha ya binadamu ambao Kristo Yesu alitaka wafuasi wake waweze kuutafakari kwa kina na mapana, kama sehemu ya hija ya maisha yao hapa duniani, ili kuonja huruma na upendo wa Baba yake wa mbinguni! Wanapaswa kutambua kwamba, ndani mwao kuna wema unaopambana na ubaya, mwanga na giza ya maisha pamoja na matamanio ambayo kamwe hawataweza kuyatekeleza. Ni watu wanaohitaji toba, wongofu wa ndani na upatanisho kadiri ya mwanga wa Injili unaofumbatwa katika huruma na upendo.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Alhamisi asubuhi, tarehe 22 Februari 2018 huko Ariccia, nje kidogo ya Roma, Mama Kanisa anapoadhimisha Kumbu kumbu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro. Anasema, Mwana mpotevu alitaka uhuru wa kuweza kuratibu maisha yake, jambo jema kabisa, lakini kwa bahati mbaya uhuru wake ulivunjilia mbali mahusiano na Baba mwenye huruma badala ya kujenga majadiliano! Alitamani raha na starehe za maisha, akagubikwa na blanketi la ubinafsi na uchoyo na hatimaye, akamezwa na malimwengu na huko akakiona cha mtema kuni kwani hakuweza kuzima ile kiu ya ndani na tamaa ya maisha na badala yake akajipalia mkaa wa majanga ya maisha.

Padre Josè Tolentino de Mendonca anakaza kusema, kiu na matamanio halali ya maisha yanaratibiwa kwa njia ya sheria, kanuni maadili na utu wema, mambo ambayo Mwana mpotevu hakuyazingatia hata kidogo. Alitakiwa kujikita katika kanuni maadili kwa kutambua uwepo wa Mungu ambao ni msaada mkubwa katika maisha. Kijana mkubwa alibaki nyumbani kwa Baba mwenye huruma, lakini daima alikosa moyo wa shukrani, kiasi hata cha kushindwa kuonja upendo wa Baba yake mambo yaliyomsababishia kupoteza dira na mwelekeo wa maisha, akawa ni mtu mwenye hasira, wivu na chuki dhidi ya mdogo wake.

Akagubikwa na ubinafsi pamoja na uchoyo usiokuwa na kifani kwa kutaka kumiliki mali yote ya Baba yake. Wivu usiokuwa na kichwa wala miguu, ukasambaratisha uhusiano wa kidugu na kuharibu maisha ya kiroho kama ambavyo pia unaweza kuvuruga mahusiano ya kifamilia, maeneo ya kazi na hata ndani ya Kanisa. Wivu ni upanga mkali unaoweza kuhatarisha mafungamano ya kijamii, kwa kukosa furaha na amani; unavunja utamaduni wa watu kukutana, kujadiliana, kuheshimiana na hata kusaidiana. Wivu ni dalili za kukosa upendo wa dhati hali inayoweza kuleta maafa makubwa. Watu wajitambue na kujikubali jinsi walivyo, tayari kujifunza kutoka katika shule ya ukarimu, ili kuwashirikisha wengine utajiri wao! Wivu ni hatari sana kwani, unapania kulipiza kisasi, hali inayomfanya mtu kukosa amani na utulivu wa ndani. Moyo wa shukrani unajenga ulimwengu bora zaidi, nje na ndani ya kila mtu!

Baba Mwenye huruma ni shule tosha kabisa ya huruma ya Mungu kwa binadamu anajitahidi kutosheleza mahitaji ya watoto wake, ili waweze kutekeleza uhuru wao pamoja na kutambua kwamba, anawapenda upeo. Anatambua atari za uhuru usiokua na mipaka pamoja na mapungufu ya watoto wake. Uhuru unapaswa kupyaishwa na kuboreshwa zaidi ili kuonja huruma na upendo wa Mungu, Huruma ya Mungu ni sanaa inayookoa maisha ambayo, waamini wanapaswa kujifunza. Si rahisi sana kutoa maana ya huruma, lakini kwa ufupi hii ni sanaa inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; upendo na mshikamano wa dhati unaoshuhudiwa katika furaha kama alivyofanya Baba mwenye huruma. Huruma ni wema, ni msamaha na upatanisho, ni zawadi na sadaka binafsi. Ni kupenda bila unafiki kwa kukubali kuganga na kuponya madonda na majeraha ya jirani zako pamoja na kuwarudishia tena ile furaha waliyoipoteza. Injili ya huruma ya Mungu inafumbata madonda ya ndani ya maisha ya mwanadamu yanayogangwa kwa divai ya upendo na uhuru kamili unaoleta mapinduzi katika maisha.

Padre Josè Tolentino de Mendonca anasema, Injili ya huruma ya Mungu inakita mizizi yake katika ukweli na uwazi, changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaigundua na kuimwilisha katika maisha yao ya kila siku. Injili ya huruma ya Mungu ni chanda na pete na furaha ya Injili na kwamba, hakuna maisha ya kweli pasi na Injili ya huruma kwani, Huruma ni Sura ya Ufunuo wa Mungu. Huruma ni dira na mwelekeo wa maisha ya kiroho na haki ya Mungu kwa binadamu inayopyaisha maisha ya watu. Injili ya huruma ya Mungu ni utamaduni wa watu kukutana ili kujenga na kukuza mchakato wa toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho. Mwenyezi Mungu ameonesha nguvu na uweza wake kwa njia ya huruma. Haya ndiyo mang’amuzi mazito ambayo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuliachia Kanisa kama amana ya maisha kiroho katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu. Huu ni ukweli wa kwanza wa Kanisa ambalo linatumwa kutangaza Injili ya huruma ambayo kwa hakika, waamini wanapaswa kuivumbua tena katika hija ya maisha yao ya kiroho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.