2018-02-22 07:53:00

Hamwezi kuzima kiu ya kiroho kwa kukumbatia vishawishi vya maisha


Waamini wanaalikwa kusikiliza kiu ya maisha yao ya ndani kwa unyenyekevu ili waweze kuizima kwa kutambua kwamba, imani ni safari ndefu yenye mabonde na milima, na siyo ngazi inayofanywa kwa njia ya watafiti wa moyo, wagunduzi au wale wanaopendeka tu! Imani ni safari endelevu inayowataka waamini kufanya hija ya maisha yao kwa kuondokana na mazoea ambayo kimsingi yana taabu na shida zake. Ugonjwa mkubwa kwa karne ya 21 ni kubweteka na kuponda mali, kwa falsafa kwamba, eti kifo chaja! Kanisa linapaswa kusafiri daima: kwa kuhubiri; kwa kusali, kwa kutafakari na kushuhudia ukweli unaomwilishwa katika vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa.

Kanisa liwe ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo na wala si kwa kuchapa maneno tu! Hii inatokana na ukweli kwamba, imani ni fadhila inayojengeka na kuimarishwa kila siku ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mzee Abramu katika Agano la Kale. Waamini wathubutu kuzima kiu yao ya ndani kutoka katika maisha yao wenyewe, daima wakitambua kwamba, hija ya maisha ya kikristo ni kufuata nyayo za Kristo Yesu.

Kama ilivyokuwa katika Agano la Kale, changamoto hazikosekani ndiyo maana Waisraeli wakamlilia Mungu na Mtumishi wake Musa kwa kutaka kuwafutilia mbali kutoka katika uso wa dunia kwa njia ya kiu na njaa. Imani kwa Mwana mpendwa wa Mungu, iwasaidie waamini kutambua karama, utajiri na mapungufu yao ya kibinadamu, kwa kujikubali, ili hatimaye, kuweza kujirekebisha kwa kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu. Kiu inatesa sana na wakati mwingine inaacha makovu ya kudumu katika maisha. Waamini wajitahidi kubadili kile wanachoweza kubadili, kwani imani peke yake haiwezi kuzima kiu ya ndani na wakati mwingine, inaweza kusababisha matatizo. Lakini, ikumbukwe kwamba, imani inamsaidia mwamini kusikia kiu inayomwezesha kuanza hija na maisha ya sala! Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumatano jioni, tarehe 21 Februari 2018 huko Ariccia, nje kidogo ya Roma.

Anafafanua kwa kusema, wakati mwingine nguvu ya Mungu inajionesha katika udhaifu kama anavyokiri Mtakatifu Paulo kwa kusema kwamba, waamini wanayo hazina kubwa ambayo imehifadhiwa katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu na wala si kutoka kwao! Waamini wanapaswa kuiishi zawadi ya imani kwa ukamilifu zaidi hata pale wanapokabiliana na udhaifu na vishawishi katika maisha, kwani hii ni njia ya kuelekea katika ukomavu wa kiutu na maisha ya kiroho. Jambo la msingi ni kuzipokea changamoto hizi na kuzifanyia kazi kama alivyofanya Mtakatifu Paulo alipoomba aondolewe mwiba katika maisha yake, lakini Mwenyezi Mungu akamjibu kwamba, neema yake ilikuwa inamtosha!

Kristo Yesu ambaye yuko ndani ya waja wake anawasaidia kujitambua, kujikubali na kuanza mchakato wa mageuzi katika maisha. Ndiyo maana Paulo Mtume anasema anapendezwa na udhaifu, ufidhuli, misiba, adha na shida kwa ajili ya Kristo, kwa maana anapokuwa dhaifu hapo ndipo alipo na nguvu. Imani inaweza kuimarika zaidi katika shida na magumu ya maisha badala ya mwamini kujiamini na kudhani kwamba, anaweza kujitosheleza katika maisha. Kusikiliza kwa makini kiu ya maisha ya ndani, ni elimu tosha katika mapambano ya maisha, kwani kiu ya maisha ya kiroho inamfundisha mwamini kujenga utamaduni wa uvumilivu.

Padre Josè Tolentino de Mendonca anakaza kusema, Kristo Yesu alijaribiwa kwa maisha yake yote na muhtasari wa majaribio haya unafumbatwa katika mambo makuu matatu: mahitaji ya kimwili, madaraka na utukufu pasi na Msalaba. Yesu aliweza kuyashinda yote haya kwa njia ya sala na kufunga. Kiu ya kweli inashibishwa na uwepo wa Mungu katika maisha. Uwepo huu unadhihirishwa kwa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee kabisa, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu: Chakula na kinywaji cha maisha ya kiroho. Waamini wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza katika maisha yao kwa upendo na uwepo wa Mungu na kamwe wasithubutu kumjaribu kama ilivyokuwa kule Masa na Meriba jangwani badala yake, wajifunze kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pale Msalabani alilia kwa sauti kubwa “Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha?”

Padre Josè Tolentino de Mendonca anawataka waamini kuchunguza dhamiri zao na kuangalia jinsi ambavyo wametumia madaraka yao katika jamii na Kanisa katika ujumla wake. Viongozi wa Kanisa wamekabidhiwa madaraka ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Utukufu wa Kristo unapata chimbuko lake katika Fumbo la Msalaba, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko. Uongozi kwa Kanisa ni huduma makini kwa watu wa Mungu unaoshuhudiwa kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani, kielelezo makini kabisa cha uhuru wa ndani. Viongozi wa Kanisa wanakumbushwa kwamba, wao ni wachungaji na wala si watawala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.