2018-02-21 10:44:00

Kiu ya Yesu: Machozi yanayogusa undani wa maisha ya mtu!


Wanawake katika shida na mahangaiko yao, wema na huruma yao katika maisha na utume wa Yesu, wamepewa kipaumbele cha pekee katika Injili. Hawa ni wanawake wanaowakilisha umati mkubwa wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa hata katika ulimwengu mamboleo katika kufikiri, kutenda na kujikita katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Wanawake ni mashuhuda wa Injili ya matumaini na mapendo, lakini bado wameendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Injili inawaonesha wanawake kuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika huduma makini bila makelele au tabia ya kujitafutia umaarufu. Mwinjili Luka anathubu kuwataja hata kwa majina, waliojitosa kimaso maso kumhudumia Kristo Yesu katika maisha na utume wake wa hadhara. Huduma ya huruma na upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni mlango wa maisha ya uzima wa milele na chemchem ya msamaha na uponyaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyojitokeza kwa yule mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili.

Bikira Maria ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo kama yanavyofafanuliwa katika Maandiko Matakatifu, kiasi hata cha kuleta mvuto kwa wanawake wenzake waliosikika wakisema, heri tumbo lililomzaa na matiti yaliyomnyonyesha Kristo Yesu. Injili ya huruma na mapendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wao kila siku ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Wanawake ni mashuhuda ya machozi yanayoashilia kiu ya maisha ya ndani, alama ya Fumbo la Umwilisho katika maisha ya waamini; Mwenyezi Mungu anapogusa udhaifu na mateso ya walimwengu. Haya ni kati ya mambo yaliyojiri katika tafakari ya Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumatano asubuhi, tarehe 21 Februari 2018 huko Ariccia, nje kidogo ya Roma.

Machozi yanayotoka kwa mgonjwa ni alama ya kutaka kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Ni mwaliko wa kutaka kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano ya kijamii hasa kwa watoto, ni kielelezo cha matumaini na imani kwa Mungu. Machozi ni sanaa inayoelezea: furaha, majonzi na matumaini yanayofumbatwa katika undani wa mtu! Kanisa lina machozi yanayofumbatwa katika Ubatizo na Sakramenti ya Upatanisho! Haya ni machozi pia yanayofumbatwa katika ushuhuda wa wafiadini na waungama imani. Mzee Nelson Mandela akiwa kifungoni, machozi yalikauka lakini bado aliendelea kuwa na kiu ya haki. Machozi ni sehemu ya utakaso wa maisha ya binadamu kuelekea katika utakatifu.

Mwinjili Luka anawaelezea wanawake kuwa ni watu walioguswa sana na maisha na utume wa Kristo Yesu, kiasi hata cha kumlilia: kielelezo cha imani na ulinzi. Mwanamke mdhambi alithubutu kuonesha upendo wake mkuu kwa Yesu kwa njia ya machozi, akaondoka kimya kimya akiwa amesamehewa dhambi zake, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha kwa njia ya huduma! Yule mwanamke alimdondoshea Yesu machozi na kuipangusa miguu yake kwa nywele zake, kielelezo cha mtumwa na huduma makini. Machozi ni kielelezo cha mateso ya ndani na jinsi ambavyo mtu anavyoguswa na matukio mbali mbali katika maisha yake! Machozi ni kiu ya imani na matumaini inayozimwa kwa uwepo wa jirani. Kilio ni kielelezo cha undani wa mtu unaohitaji kutakaswa kwa kuambatwa na imani thabiti, upendo na ukarimu kama ulivyoshuhudiwa na Kristo Yesu kwa yule mwanamke mdhambi! 

Hata leo hii, anasema Padre Josè Tolentino de Mendonca, Yesu anawataka wafuasi wake kumwangalia yule mwanamke mdhambi kwa jicho la imani na mapendo; ukarimu, ukweli na uwazi; toba na wongofu wa ndani. Yule mwanamke mdhambi alikuwa ametenda makubwa zaidi kuliko hata Simoni kushindwa kumpatia Yesu maji ya kuosha miguu yake, busu wala mafuta. Mwanamke mdhambi akarejea nyumbani kwake akiwa ametakasika kwa kusamehewa dhambi zake. Haya ndiyo machozi ambayo ni chapa inayopaswa kuacha alama ya kudumu katika maisha ya waamini wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.