2018-02-20 06:59:00

Ushirikiano na mshikamano katika huduma ya maendeleo endelevu!


Mnamo tarehe 5 Februari 2018 yalitiwa mkwaju Makubaliano ya ushirikiano wa Uinjilishaji kati ya majimbo makuu ya Seoul, Corea ya kusini na Ouagadougou, Bukirna Faso. Makubaliano hayo yanalenga kukuza huduma za afya na elimu. Jimbo kuu la Seoul kwa miaka mitatu ijayo litakuwa na mipango na miradi kadhaa kwa ajili ya kusaidia jimbo kuu la Ouagadougou, ambapo waseminari kadhaa watakuwa wanapelekwa kimalezi katika seminari ya taalimungu jimboni Seoul, na pia misaada katika sekta ya afya kwa ushirikiano mahususi kati ya Hospitali ya Bikira Maria ya Seoul na Hospitali Mwenyeheri Paulo VI ya Ouagadougou.

Kardinali Andrew Yeom Soo-jung, Askofu mkuu wa Seoul anasema, neno communio linatokana na maneno mawili ya Kilatini, cum na manus, ambayo yana maanisha kushirikishana dhamana. Kumbe ni malengo ya majimbo haya mawili kushirkiana katika kuboresha dhamana ambayo Kanisa katika maeneo hayo limekabidhiwa sanjari na mpango mzima wa Uinjilishaji wa mtu, kiroho na kimwili. Kwa upande wake Kardinali Philippe Ouédraogo, Askofu mkuu wa Ouagadougou anasema, anatoa shukrani na kuthamini sana ushirikiano kati ya majimbo hayo mawili, ambayo ni ishara kubwa ya mageuzi ya kimtazamo na ukomavu wa kiimani, kwani awali ilizoeleka misaada ya namna hiyo kuwa inatokea barani Ulaya, na sasa anashuhudia uwezekano wa mshikamano wa namna hiyo kutoka nchi ya Corea, barani Asia.

Katika safari hiyo nchini Bukirna Faso, kwa muda wa siku 6, Kardinali Andrew Yeom Soo-jung, aliongozana na Askofu Koo Yo-bi, Askofu msaidizi wa Seoul, na Professa Kim Young-sik, Mwenyekiti wa Hospitali ya Mt. Maria ya Seoul. Wakiwa nchini humo, Kardinali Andrew Yeom Soo-jung alipata fursa ya kushiriki maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Madhabahu ya Yagma, akabariki gari la wagonjwa iliyozawadiwa kwa Hospitali ya Mwenyeheri Paulo VI Ouagadougou, na kisha Kardinali Andrew Yeom Soo-jung alikutana na Rais Roch Marc Christian Kabore wa Bukirna Faso.

Itakumbukuwa kwamba, Kardinali Andrew Yeom Soo-jung na Kardinali Philippe Ouédraogo waliteuliwa na kutunukiwa hadhi ya kuwa makardinali siku moja mnamo mwezi februari 2014, kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Mwaka huo huo wakati Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Corea, Kardinali Philippe Ouédraogo alialikwa, na akaalikwa tena mwaka 2017 wakati Monsinyo Koo Yo-bi alipowekwa wakfu na kuwa Askofu msaidizi wa Seoul. Kwa hakika hizi ni ishara nzuri za mahusiano na mshikamano bora kati ya majimbo haya mawili.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.