2018-02-19 08:46:00

Papa Francisko: Vijana 300 kushiriki katika utangulizi wa Sinodi!


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 18 Februari 2018 alitangaza kwamba, kuanzia tarehe 19 Machi 20018, yaani Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu Mchumba wake wa Bikira Maria, hadi tarehe 24 Machi 2018, Jumamosi kabla ya kusherehekea Siku ya Vijana Kijimbo, Jimbo kuu la Roma litakuwa na ugeni mzito wa vijana zaidi ya 300 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaokuja ili kushiriki maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Baba Mtakatifu anawataka vijana wote kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maandalizi haya, kwa kutambua kwamba, wao ndio wadau na wahusika wakuu wa Sinodi ya Vijana. Vijana wanaweza kuchangia mawazo yao kwa njia ya mitandao ya kijamii kadiri ya lugha zao, kazi itakayoratibiwa na vijana wenzao. Lengo ni kujenga mtandao wa vijana katika mitandao ya kijamii, ili kushiriki kikamilifu na wale vijana walioteuliwa kuwawakilisha vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaokuwa hapa mjini Roma. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kutembelea katika tovuti ya Sekretarieti ya Baraza kuu la Sinodi za Maaskofu ili kupata maelezo zaidi. Anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza vijana kwa mchango wao unaoliwezesha Kanisa kufanya hija pamoja nao.

Papa Francisko amekumbusha tena kwamba, Kwaresima ni Kipindi cha toba na wongofu wa ndani; ni wakati wa mapambano ya maisha ya kiroho. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee, wafungwa, kwa kuwatia shime kukiishi Kipindi cha Kwaresima kama muda muafaka wa upatanisho na upyaisho wa maisha ya kiroho, chini ya jicho la huruma ya Mungu. Amewaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumkumbuka na kumsindikiza, yeye pamoja na viongozi wa Sekretarieti kuu ya Vatican, walioanza Mafungo ya Mwaka, huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma, ili kujipatia muda zaidi wa kusali na kutafakari, tayari kukabiliana na changamoto za maisha na utume wao, wanapojiandaa kuadhimisha Fumbo la Pasaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.