2018-02-19 15:46:00

Kristo Yesu ndiye anayezima kiu ya ndani ya maisha ya waamini wake!


Padre Josè Tolentino de Mondonca katika tafakari yake ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumapili jioni, tarehe 18 Februari 2018 anasema, Injili ya furaha na huruma ya Mungu, ndiyo inayozima kiu ya watu walioko pembezoni mwa maisha ya jamii! Mkazo ni kuhusu ”Heri za Kiu” yaani: kiu ya kupenda na kupendwa; kutambua na kutambulikana; mahusiano; utu na heshima; majadiliano, ukweli na uwazi; kiu ya utu na ubinadamu, lakini zaidi ni kiu ya kutaka kumwona Mungu kama ilivyokuwa kwa Mwanamke Msamaria aliyeomba maji ambayo yangekuwa ndani mwake chemchemi ya maji yanayobubujikia uzima wa milele. Mwanamke Msamaria akamfungulia Yesu hazina ya moyo wake. Hii inaonesha “Heri ya Kiu” inayozimwa kwa kukutana na Kristo Yesu katika maisha kama ilivyotokea kwa yule Mwanamke Msamaria pale kisimani.

Uchovu wa Yesu unawakirimia watu fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu. Wasamaria ambao walihesabiwa kuwa “si mali kitu” watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, wakabahatika kukutana na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Nguvu ya Mwana wa Mungu anasema Mtakatifu Agostino, imeumba na udhaifu wa Kristo Yesu umewakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu anaonesha kwamba, ni Mwalimu na Bwana; ni mwingi wa huruma na mapendo; anayesubiri kwa matumaini makubwa, watu kumkimbilia tena katika maisha yao!

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele amekuja ulimwenguni ili kuonesha mshikamano na binadamu sanjari na kuwatafuta wadhambi. Anataka kuzima kiu ya ndani kabisa katika maisha ya mwanadamu, ili kulowanisha “jangwa la maisha ya kiroho”, kwa kuponya na kuganga majeraha ya mwanadamu yanayofumbatwa katika kinzani kama ilivyokuwa kwa Wasamaria na Waisraeli. Njaa na kiu kubwa ya Yesu ilikuwa ni kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, jibu makini linaweza kutolewa kwa waamini kwa kujiaminisha pamoja na kuwa na ujasiri kama aliokuwa nao yule Mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, kwa ujasiri wake akapata kuona tena!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na Haki”  anasema, msamaha ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha, kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambao ni huruma ya milele inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini ya maisha mapya yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha bado yanasheheni matatizo na changamoto mbali mbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi! 

Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu; sala ambayo inapaswa kumwilishwa katika matendo. Waamini wajifunze kuombeana huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu anasema Padre Josè Tolentino de Mendonca katika tafakari yake ya kwanza, kwani hata sala zao zinapaa kama moshi wa ubani, hadi mbinguni licha ya magonjwa yao ya maisha ya kiroho na ukosefu wa kinga za maisha ya kiroho mwilini, yaani: UKIRO. Hii inatokana na ukweli kwamba, ndani mwao wanayo neema ya Mungu.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 18 - 23 Februari 2018, watasitisha shughuli zote za kitume na kwenda “kujichimbia Mlimani”, kwenye nyumba ya mafungo ya “Divin Maestro” huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma, ili kujipatia muda wa kusali na kutafakari tayari kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.