2018-02-19 16:08:00

Kiu na njaa ya maisha ya kiroho inavyoweza kuleta kasheshe!


Padre Josè Tolentino de Mondonca katika tafakari yake ya Pili kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumatatu, asubuhi 19 Februari 2018, amekazia kwa namna ya pekee: Sayansi ya kiu; Maji yanayoweza kuzima kiu ya ndani ya maisha ya mwanadamu; mateso na mahangaiko ya kiu ya mwanadamu; mfano wa kiu ya mwanadamu na hija kuelekea katika kuzima kiu hii hata kama ni kwa kiasi kidogo tu cha maji! Sayansi ya kiu kama inavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu inajikita katika kiu ya “maji ya uzima wa milele”, “kiu ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; pamoja na “kiu ya imani na matumaini” ya kumwona Mwenyezi Mungu.

Padre Josè Tolentino de Mondonca  anawataka waamini kutambua kiasi cha maji wanachohitaji ili kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho, kwa kujifunza kumfahamu Mwenyezi Mungu, ili kumsikiliza kwa ari na moyo mkuu. Mwanadamu anao uwezo wa kutambua kiu katika maisha yake kwani haya ni mateso na mahangaiko ya watu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli kule Masa na Meriba, jangwani, watu walipomnung’unikia Mungu na Musa kutokana na maumivu makali ya kiu! Kiu inaweza kusababisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, hali inayoonesha udhaifu wa maisha ya binadamu. Si rahisi sana kwa mwanadamu kuvumilia kiu kwa muda mrefu.

Padre Josè Tolentino de Mendonca  anaendelea kufafanua kwamba, kiu na njaa ni mambo yanayohatarisha maisha ya binadamu. Haya ni mambo yanayogusa mambo msingi katika undani wa mwanadamu, yaani maisha ya kiroho, kiasi cha kumnyima mwamini furaha ya kweli katika maisha. Katika changamoto hii, Kristo Yesu anaendelea kuwaalika wafuasi wake kumwendea kwa moyo wa imani na matumaini ili aweze kuzima kiu ya maisha yao ya ndani, yaani kiu ya maisha ya uzima wa milele!

Anasema, Mtakatifu Exupèry katika kitabu chake alichoandika kunako mwaka 1943, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia anazungumzia kuhusu hija ya maisha ya kiroho “peregrinatio animae” ili kuweza kuzima kiu yake ya ndani, akitambua kwamba, hapa duniani hana makazi ya kudumu, daima ataendelea kuwa ni mpita njia akiwa na kumbu kumbu hai inayomsukuma katika toba na wongofu wa ndani unaomwilishwa katika matendo ya huruma. Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuwaita wale wote wenye kiu ya maji ya uzima wa milele wajongee kwake ili aweze kuizima kabisa.

Kristo Yesu kwa kutambua umuhimu wa chakula katika maisha ya watu, akaweka adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni kiini na hatima ya maisha na utume wa Kanisa. Meza ya Neno na Ekaristi ni mahali pa kushirikishana maisha ya uzima wa milele, kielelezo cha ukarimu na upendo kwa jirani. Hapa ni mahali pa kujenga na kudumisha mahusiano na mshikamano wa dhati. Chakula kinapaswa kuwa ni tendo la kijumuiya linalotakiwa kupewa heshima yake. Kuwanywesha wenye kiu ni sehemu pia ya matendo ya huruma yanayogusa undani wa maisha ya watu. Kiu hii inaweza kuwa ni kiu ya mahusiano, ya kukubalika mbele ya watu wengine au kiu ya kupenda na kupendwa. Padre Josè Tolentino de Mendonca  anahitimisha tafakari yake kwa kusema kwamba, mwanadamu katika maisha yake, anabeba aina mbali mbali za kiu, ambayo kimsingi ni hazina na amana wanayopaswa kuitambua, ili hatimaye, waweze kuipeleka mbele ya Mwenyezi Mungu kwa moyo wa shukrani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.