2018-02-16 06:35:00

Papa Francisko na wasaidizi wake "kujichimbia" mlimani kwa mafungo!


Padre Josè Tolentino de Mondonca ndiye aliyekabidhiwa dhamana ya kumpandisha Baba Mtakatifu Francisko na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Vatican ili kusali, kutafakari na kufunga wakati wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2018. Katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi anayeonesha sifa za ubaba, katekista na mchungaji mkuu, anayejisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu. Yeye ni sauti ya kinabii katika kutetea haki msingi za binadamu; utu na heshima yake kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ni kiongozi anayeonesha ujasiri kiasi cha kuwashangaza wengi katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Amethubutu kuishi katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu, ama kwa hakika ni mtu wa watu kwa ajili ya watu, pamoja na kati ya watu! Ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Padre Josè Tolentino de Mondonca anasema, alipoombwa na Baba Mtakatifu kuwaongoza kwa tafakari na mafungo kwa mwaka 2018, alilipokea ombi hili kwa moyo wa unyenyekevu na kuiona kuwa ni changamoto pevu katika historia ya maisha na utume wake kama Padre.

Akaamua kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, anakata kiu ya wasikilizaji wake, kwa kuwawekea mbele yao Kristo Yesu, ili waweze kujichotea nguvu kutoka kwake, tayari kutoka kifua mbele kwenye kutangaza Injili ya furaha na huruma ya Mungu, inayozima kiu ya watu walioko pembezoni mwa maisha ya jamii! Anapenda kukazia kuhusu ”Heri za Kiu” yaani: kiu ya kupenda na kupendwa; kutambua na kutambulikana; mahusiano; utu na heshima; majadiliano, ukweli na uwazi; kiu y autu na ubinadamu, lakini zaidi ni kiu ya kutaka kumwona Mungu!  Yesu baada ya kuhukumiwa na kusulubiwa Msalabani, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema ”Naona kiu”. Haya ndiyo maneno yaliyotamkwa na Yesu kabla ya kukata roho!

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 18- 23 Februari 2018, watasitisha shughuli zote za kitume na kwenda “kujichimbia Mlimani”, kwenye nyumba ya mafungo ya “Divin Maestro” huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma, ili kujipatia muda wa kusali na kutafakari tayari kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Ni muda wa kwenda jangwani ili kujichotea nguvu za maisha ya kiroho, tayari kupambana na changamoto mamboleo! “Masifu ya Kiu” ndiyo tema iliyochaguliwa na Padre Josè Tolentino de Mondonca, Kaimu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki, Lisbon nchini Ureno na ni Mshauri katika Baraza la Kipapa la Utamaduni.

Padre Josè Tolentino de Mondonca alizaliwa kunako mwaka 1965, baada ya masomo na majiundo yake ya kipadre, kunako mwaka 1990, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kimsingi, yeye ni mtaalam aliyebobea katika masuala ya kitaalimungu na fasihi simulizi. Kunako mwaka 2014 alitambulishwa rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mashairi Duniani. Mafungo haya yataanza Jumapili jioni tarehe 18 kwa tafakari ya utangulizi, Ibada ya Kuaabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Masifu ya jioni. Siku zinazofuatia, zitafunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayowashirikisha wana mafungo wote, tafari ya kwanza, tafakari ya pili wakati wa alasiri, Masifu ya jioni na Ibada ya Kuabudu Ekaristi. Ijumaa, tarehe 23 Februari 2018 kutakuwepo na mabadiliko kidogo, kwani siku hiyo kutakuwa na tafakari moja na hatimaye, kuhitimisha mafungo, tayari, Baba Mtakatifu Francisko na waandamizi wake, kurejea tena mjini Vatican kuendelea na utume wao.

Padre Josè Tolentino de Mondonca, anasema, katika tafakari zake anapenda kuwasaidia wale wanaofunga kushangaa na baadaye, ataendelea kutafakari kuhusu sayansi ya kiu, kwani anatambua kwamba, hata yeye mwenyewe ana kiu ya kutaka kuonana na Kristo Yesu. Machozi yanayobubujika yanaonesha kiu ya kutaka kumwona Yesu. Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu kuzima kiu ya maisha yao kutoka katika undani wao; aina mbali mbali ya kiu pamoja na changamoto ya kusikiliza kiu ya watu wanaoishi pembezoni mwa jamii. Kama ilivyo desturi, wakati wote wa Mafungo ya Kiroho, shughuli zote zinazofanywa na Baba Mtakatifu zinasitishwa, kumbe, hakutakuwepo na mikutano ya hadhara na binafsi wala Katekesi kwa siku ya Jumatano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.