2018-02-13 08:11:00

Changamoto ya wakimbizi wa Rohingya ipate suluhu ya haki na dumifu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 12 Februari 2018 amekutana na kuzungumza na Bi Sheikh Hasina, Waziri Mkuu wa Bangladesh pamoja na ujumbe wake, ambaye baadaye pia, amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Bi Hasina, wote wawili wameridhishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Bangladesh na kwa namna ya pekee, wameridhishwa na mafanikio makubwa yaliyopatikana wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bangladesh.

Hili ni tukio ambalo liliwashirikisha watu wa Mungu nchini Bangladesh na kwamba, limeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu hawa! Baadaye, wamejadili pia mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wanachi wa Bangladesh, hususan katika sekta ya elimu, mchango wa serikali katika kukuza na kudumisha uhusiano mwema kati ya Jumuiya mbali mbali za kidini nchini humo sanjari na kulinda haki za makundi ya watu wachache na wahamiaji. Baba Mtakatifu ameridhishwa na jinsi ambavyo Serikali ya Bangladesh inavyojitahidi kutoa huduma kwa wakimbizi wa Rohingya; ni matumaini yake kwamba, suluhu ya haki na yenye kudumu itaweza kupatikana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.