2018-02-10 07:49:00

Waonjesheni wagonjwa: huruma, upendo, utu na heshima!


Kila mwaka, tarehe 11 Februari, kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, Kanisa huadhimisha siku ya wagonjwa duniani. Ni maadhimisho yanayotualika kama Kanisa kuangaza jicho la pekee kwa fumbo la ugonjwa katika maisha ya mwanadamu na kwa wagonjwa walio katika jumuiya zetu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa siku hii ya leo unaongozwa na kauli mbiu “Mama tazama Mwanao. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani  mwake”. Kati ya mengi anayoeleza Baba Mtakatifu katika ujumbe huu ni mkazo juu ya utu, heshima na mahitaji msingi ya wagonjwa vitu ambavyo taasisi za afya pamoja na wote wanaohusika na tiba kwa wagonjwa wanapaswa kuvipa kipaumbele. Maandiko Matakatifu yanayotuongoza katika tafakari ya leo ya Neno la Mungu ni yale ya dominika ya 6 ya mwaka. Yanadokeza dhamira ya Huruma ya kimungu kwa wahitaji katika jumuiya zetu.

Masomo kwa Ufupi

Somo la Kwanza (Wal. 13: 1-2, 45-46) linaeleza mojawapo ya mapokeo ya Wayahudi kuhusu kanuni za usafi za kiibada. Kanuni zilizokuwa zikieleza ni yupi anayestahili kushiriki pamoja na jumuiya katika ibada na ni yupi aliye najisi asiyestahili kushiriki. Mapokeo yanayoelezwa na somo la leo ni yale yaliyohusu ugonjwa wa ngozi tunaoweza kuuita ukoma. Mgonjwa wa ukoma na yeyote aliyekuwa na dalili hizo alitengwa na jumuiya na hakutakiwa kumsogelea asiye na ukoma. Hakuruhusiwa kushiriki shughuli zozote za jumuiya na endapo mtu asiye mkoma angemgusa au kumkaribia basi na yeye angetengwa. Na walitengwa hadi hapo kuhani atakapithibitisha kuwa ugonjwa umeisha. Ugonjwa huu haukuhusishwa moja kwa moja na dhambi japo kuwa kuna watu ambao Mungu aliwaadhibu kwa ukoma kutokana na makosa yao. Kwa nini walitengwa? Sababu kubwa ya kuwatenga wagonjwa wa ukoma ni ile ya kiibada, yaani kulinda utakatifu (usafi) wa ibada kwa Mungu lakini pia kuepuka kuwaambukiza wengine. Maambukizi haya yaliyoepukwa ni yale ya kimwili (ugonjwa) lakini pia ya kimaadili hasa pale ambapo ukoma ulitokana na adhabu ya Mungu kwa makosa ya kimaadili.

Somo la pili (1Kor. 10:31 - 11:2) Mtume Paulo anatoa mwongozo kwa Wakorintho katika mazingira yanayofanana na ya Wayahudi katika somo la kwanza. Katika Korintho, kama katika maeneo mengine ya dola ya Kirumi, kulikuwa na ibada kwa miungu wengi. Ibada hizi ziliendana na kutolea sadaka za wanyama ambapo nyama hizo baadae watu walizila. Inawezekana pia kuwa zilikuwa zinapatikana masokoni. Wakristo waligawanyika juu ya suala hili. Wapo waliokuwa wanasema ni halali kula nyama hizi na wapo walikuwa wanasema si halali. Hapo awali Mtume Paulo aliwaandikia na kuwaambia kuwa miungu si Mungu na kinachotolewa kwao ni kama mchezo wa kuigiza. Kumbe wale ambao dhamiri zao ziko imara wanaweza kula nyama hizo bila kuharibu imani yao (1Kor. 8:5). Katika somo la leo, Mtume Paulo anakaza kuwa katika kuenenda hivyo wawe makini wasiwakwaze wale wale dhamiri dhaifu. Kumbe katika kuepuka kuwakwaza wengine mkristo anaweza asile nyama hizo kwani kuzila au kutokuzila hakuathiri imani yake. Anawaeleza wakorinto kuwa msimamo huo anaowapa ni msimamo aliouiga toka kwa Kristo, kufanya yote kwa sifa na utukufu wa Mungu na kwa kuangalia mafaa ya walio dhaifu. Kisha anawaalika wao pia wamuige yeye kama anavyomuiga Kristo.

Somo la Injili (Mk. 1:40 - 45) linaonesha huo msimamo wa Yesu ambao Mtume Paulo anauzungumzia, msimamo tunaoweza kuuita Huruma ya Mungu. Ni kwa msimamo huu wa huruma Kristo anavunja kanuni ya Wayahudi ya kutomkaribia wala kuzungumza na mwenye ukoma. Yesu anamkaribia, anazungumza naye na anamponya kisha anamtuma ajioneshe kwa kuhani ili aruhusiwe kujiunga tena na jumuiya. Injili inaonesha pia kuwa huruma hii ya Yesu isiyo na mipaka haipaswi kuwekewa mipaka na sala ya mwombaji. Mwenye ukoma anasema “ukitaka waweza kunitakasa” na hapo hapo akitufundisha nasi namna ya kusali na namna ya kuijongea huruma ya Mungu.

Katika siku hii ya Wagonjwa ujumbe wa Baba Mtakatifu na tafakari ya Maandiko Matakatifu ya leo vinaungana kutualika tuwatizame, tuwapokee na tuwahudumie wagonjwa kwa Huruma. Ni kwa kusukumwa na huruma hii Kanisa kwa zaidi ya miaka 2000 limeunganisha katika utume wake uinjilishaji huduma kwa wagonjwa. Limeanzisha na kusimamia taasisi mbalimbali za afya na kuhusika kuwaandaa na kuwapa miongozo wale wanaohusika na tiba na huduma mbalimbali kwa wagonjwa. Huruma hii kwa wagonjwa iendelee kutawala katika taasisi hizi ili kweli zijikite katika utu, heshima na mahitaji ya msingi ya wagonjwa pale zinapowahudumia. Ni muhimu sana pia kuzikinga taasisi hizi na maelekeo ya kibiashara na yote yanayofifisha hadhi na heshima ya wagonjwa. Jukumu hili ambalo Kanisa linachukua kwa nafasi ya kwanza kama anavyotualika Baba Mtakatifu linapaswa kuungwa mkono na wadau wote wa huduma hii na kwa namna ya pekee serikali. Serikali hazipaswi kuziona taasisi za Kanisa za afya kama washindani wa taasisi zake bali kama washiriki pamoja nazo katika kuwahudumia watu waliokabidhiwa na Mungu. Ni kwa ushirikiano huu huduma ya tiba itamweka mwanadamu katika nafasi na heshima yake.

Huruma kwa wagonjwa itusogeze karibu nao. Kama alivyowahi kutukumbusha Baba Mtakatifu Fransisco, “muda tunaotumia kwa wagonjwa ni muda mtakatifu”. Tuwatembelee, tuwasalimu, tuzungumze nao na hata katika magonjwa ya muda mrefu tusiwakimbie na kuwaacha peke yao. Bikira Maria ambaye uchungu kama upanga uliupenya moyo wake lakini haukumvunja moyo atufundishe kuupokea uchungu wa ugonjwa katika maisha yetu bila kuvunja moyo wa imani na matumaini kwa Mungu mwokozi wetu.

Padre William Bahitwa

VATICAN NEWS.








All the contents on this site are copyrighted ©.