2018-02-09 07:10:00

Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018, Jimbo kuu la Dublin, Ireland


Baba Mtakatifu Francisko anasema, familia bado inaendelea kuwa ni kitovu cha Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu, kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo ambao umegeuka kuwa kama tambara bovu! Ni wajibu wao kutangaza na kushuhudia uzuri, utakatifu na heshima ya maisha ya ndoa na familia kama njia muafaka ya kuyatakatifuza malimwengu! Familia kadiri ya mpango wa Mungu kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu na familia jinsi ilivyo katika ulimwengu mamboleo ni changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Injili ya familia!

Siku ya IX ya Familia Duniani itaadhimishwa Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland, kuanzia tarehe 22- 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”. Maandalizi haya yanaongozwa kwa namna ya pekee kabisa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi.

Lakini, ikumbukwe kwamba, Neno la Mungu ni sawa na upanga wenye makali kuwili; hata familia zinaweza kuwa ni chemchemi ya furaha na upendo wa dhati unaobubujika kutoka kwenye huruma ya upendo wa Mungu. Lakini pia, familia zisipokuwa makini zinaweza kuwa ni mahali pa patashika nguo kuchanika, mahali pa vipigo vya majumbani na mahali ambapo wanawake na watoto hawatambuliwi wala kuthaminiwa utu na heshima yao! Hivi karibuni, Kardinali Kevin Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha akiwa ameandamana na  Dr. Marco Tibaldi, Mshauri wa masuala ya kitaalimungu katika Baraza hili la kipapa, amewasilisha Katekesi za kimataifa mintarafu maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani, huko Dublin, ili kuwawezesha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kuhusu “Mradi mkubwa wa Fumbo la Upendo”.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Machi 2017 alitoa mwongozo makini ambao unapaswa kufuatwa kama sehemu ya tafakari ya Wosia wa Kitume, "Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Swali la msingi hapa ni kujiuliza ikiwa kama Injili inaendelea kuwa ni sababu ya furaha kwa ulimwengu? Je, Familia bado inaendelea kuwa ni Habari Njema kwa ulimwengu mamboleo? Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, ni kweli familia inaendelea kuwa ni sababu ya furaha na Habari Njema kwa walimwengu, kwani, uhakika huu unafumbatwa katika mpango wa Mungu kwa mwanadamu; upendo ambao unapaswa kupewa jibu la “Ndiyo” na viumbe vyote kwani hiki ni kiini cha moyo wa binadamu.

Hii ni “Ndiyo” inayowaunganisha bwana na bibi katika maisha ya ndoa na familia tayari kushiriki katika mchakato wa kuhudumia uhai katika hatua zake zote! Hii ni “Ndiyo” ya Mungu inayodhihirisha ile dhamana yake kwa binadamu aliyejeruhiwa, anayetendewa vibaya na kutawaliwa na ukosefu wa upendo. Familia kimsingi ni “Ndiyo” ya upendo wa Mungu. Upendo ni chimbuko ambalo linaiwezesha familia kushuhudia, kuzalisha na hatimaye kuzamisha upendo wa Mungu duniani. Bila upendo huu, si rahisi sana kuweza kuishi kama watoto wa Mungu, watu wa ndoa, wazazi na kama ndugu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuhimiza umuhimu wa familia kuishi kwa kujikita katika upendo kwa ajili ya upendo na ndani ya upendo wenyewe. Hii ina maana kwamba wanandoa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusameheana, kuvumiliana na kuheshimiana.

Baba Mtakatifu anawaalika wanafamilia kumwilisha ndani mwao maneno makuu matatu: “Hodi, samahani na asante”. Mama Kanisa kila wakati anapata mang’amuzi ya udhaifu wa binadamu, ndiyo maana watu wote, familia pamoja na viongozi wa Kanisa wanapaswa kujenga tabia ya unyenyekevu uliopyaishwa, unaotamani kufundwa vyema; kuelimishwa ili uweze kuelimisha; kusaidiwa ili uweze kusaidia; kusindikiza, kung’amua, kuwaingiza na kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho na ushuhuda wa mradi mkubwa wa upendo wa Mungu kwa binadamu! Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, anaota ndoto ya kuona Kanisa lisilojitafuta lenyewe, bali Kanisa linalotoka kwenda kuwatafuta watu waliojeruhiwa; Kanisa lenye huruma linalotangaza na kushuhudia upendo wa Mungu ambao ni chemchemi ya huruma, unaowapyaisha watu, ili kweli familia za Kikristo ziweze kuwa ni madhabahu ya huruma na shuhuda wa huruma ya Mungu.

Baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani, huko Dublin, itakuwa tena ni fursa ya kumwilisha mikakati hii katika uhalisia wa maisha ya watu! Mafundisho ya Wosia “Furaha ya upendo ndani ya familia” yanapaswa kupewa msisitizo wa pekee, kwani, Kanisa linatamani kuwaona wanandoa wakiwa daima katika hija ya maisha ya kiroho yanayomwilishwa katika ukweli wa maisha na wala si katika ndoto na hali ya kufikirika. Ndiyo maana anasema Kardinali Kevin Farrell kwamba, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limepewa dhamana ya kuwaandaa kikamilifu wanandoa watarajiwa kwa kuhakikisha kwamba, wanapewa katekesi makini na endelevu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya Ndoa na familia, daima wakijitahidi kuiga mfano bora wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Luka 2:41-52 ndicho kiini cha Injili ya familia mintarafu Familia Takatifu ya Nazareti.

Katekesi hizi zinalenga kuipembua hali ya maisha na familia katika ulimwengu mambaoleo; umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya Ndoa na familia; namna ya kuweza kutekeleza ndoto ya Mungu katika maisha ya ndoa na familia; udhaifu wa maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kujikita katika utamaduni mpya unaofumbatwa katika Injili ya familia sanjari na Injili ya matumaini na Furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kila katekesi inafunguliwa kwa sala na kuhitimishwa kwa maswali dodoso yanayoweza kujadiliwa ndani ya familia na kwenye Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Katekesi hizi zinaweza kupatikana kwenye mtandao wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia tarehe 2 Februari 2018 kwa anuani ifuatayo: www.laityfamilylife.va Waamini na watu wenye mapenzi mema pia wanaweza kusikiliza kutoka kwenye You Tube ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.