2018-02-09 07:34:00

Sera na mikakati ya kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi duniani


Tamko la New York kuhusu wakimbizi na wahamiaji linabainisha umuhimu wa mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaolazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Hii ni changamoto kubwa kwani takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya bilioni moja wamo katika mchakato wa kutafuta hifadhi kama wakimbizi au wahamiaji. Hii inatokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na utandawazi usiokuwa na uwiano bora.

Wahamiaji halali wana mchango mkubwa katika ustawi wa nchi wanakotoka na kuhamia, kwa kupata ajira zinazowawezesha kuchangia katika maendeleo ya nchi zinazowapatia hifadhi. Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi haramu ni dalili kwamba, njia halali za uhamiaji hazijapata mafanikio makubwa katika Jumuiya ya Kimataifa. Hata kama wimbi la wahamiaji haramu ni jambo la mpito, lakini madai makubwa yamekuwa ni usalama wa raia na mali zao, hali ambayo inapaswa kutazamwa kwa mwelekeo chanya zaidi, kwa kukazia: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss wakati akichangia hoja kuhusu “wahamiaji haramu na njia za uhamiaji halali” kama sehemu ya mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa inayoandaa Mkataba wa Kimataifa kuhusu usalama wa wahamiaji na wenye mpangilio thabiti. Kutokana na mwelekeo wa ubaguzi, wasi wasi pamoja na kukosa imani na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu hatima yao, mara nyingi wakimbizi na wahamiaji wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo na kazi za suluba, mambo yanayo dhalilisha utu na heshima yao kama binadamu pamoja na haki zao msingi. Ni watu wasiojulikana kisheria na matokeo yake, hawawezi kuheshimiwa wala kuthaminiwa hata kidogo!

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anakiri umuhimu wa Serikali husika kulinda mipaka ya nchi yake na kuratibu wimbi la wakimbizi na wahamiaji, lakini pia inapaswa kuwa na mfumo bora wa sheria unaoratibu na kusimamia shughuli za wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia: utu wao kama binadamu na haki zao msingi, kipaumbele cha kwanza wakiwa ni wanawake, watoto na wazee. Hapa sheria, mikataba na itifaki za kimataifa hazina budi kuzingatiwa na vyonmbo vya sheria katika nchi husika. Pili kuna haja ya kukazia sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutumiwa kama njia halali za uhamiaji badala ya kuendekeza sheria na taratibu ambazo si rafiki sana kwa utu na heshima ya binadamu!

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushughulikia changamoto ya wakimbizi na wahamiaji katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa kuongeza fursa ya watu kupata vibali halali vya uhamiaji hali ambayo inaweza pia kuchangia uhusiano mwema na jumuiya mahalia, mambo yanayosimikwa katika utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kama ndugu badala ya kujenga hofu zisizo na mashiko dhidi ya wahamiaji, hali inayochangia ubaguzi, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wakimbizi na wahamiaji duniani. Usalama, utu na mahitaji msingi ni mambo ambayo yanatiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu wakimbizi na wahamiaji duniani.

Ikumbukwe kwamba, wahamiaji na wakimbizi ni sehemu muhimu sana katika ulimwengu wa utandawazi, changamoto ni kuhakikisha kwamba, watu hawa wanaweza kuungana tena na familia zao, kama sehemu ya haki zao msingi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia husika. Hapa kunahitajika ujenzi wa mshikamano, umoja na udugu wa kimataifa ili kuunda mazingira yatakayowawezesha watu kubaki katika nchi zao na wala si kulazimika kuzikimbia au kuhama kutokana na mashinikizo mbali mbali.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anahitimisha hoja zake kwa kukazia kuwa hakuna shaka kwamba, uhamiaji ni kati ya nguvu muhimu sana inayotoa taswira ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kijamii katika ulimwengu mamboleo. Umefika wakati wa kutoa mwelekeo chanya zaidi kuhusu mchango wa wakimbizi na wahamiaji katika ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, hasa pale wahamiaji hawa wanapokuwa wameungana na familia zao, ili dhana hii iweze kuingizwa katika Mkataba wa Kimataifa kuhusu usalama wa wahamiaji na wenye mpangilio thabiti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.