2018-02-09 17:02:00

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Utume


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 10 Februari 2018 kuanzia saa 11:30 majira ya jioni kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, yenye makao yake makuu mjini Roma. Jumuiya hii ilianzishwa kunako tarehe 7 Februari 1968 kwa kujikita katika Sala, Maskini na Amani duniani; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa.

Tunu hizi msingi anasema Bwana Marco Impagliazo, Rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, zinaendelea kuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio sehemu mbali mbali za dunia kwa kuwashirikisha wanachama zaidi ya sitini elfu kutoka katika medani mbali mbali za kijamii, umri na uwezo wao ndani ya jamii. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo, furaha na matumaini kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Jumuiya hii katika kipindi cha miaka 50 ya uhai wake, imekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa maskini; watu wasiokuwa na makazi rasmi; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi Barani Afrika na Amerika ya Kusini; bila kusahau huduma ya elimu kwa watoto wanaofundwa katika “Shule ya Amani”. Jumuiya imeendelea pia kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa UKIMWI kwa njia ya utekelezaji wa Miradi ya “The Dream” pamoja na BRAVO”. Majadiliano ya kidini na kiekumene yamekuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake, mintarafu ari, moyo na changamoto zilizotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa mkutano wa kuombea Amani Duniani, tarehe 4 Oktoba 1992. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ndiyo iliyochangia kwa kiasi kikubwa hata kusitishwa kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji. Imekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji hawa wanashirikishwa kikamilifu katika maisha ya jamii inayowakirimia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.