2018-02-08 08:47:00

Papa: Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni donda ndugu mamboleo


Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa, katika kazi za suluba, ukahaba, biashara haramu ya viungo vya binadamu, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge; matendo yote haya ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na yanapaswa kutambulika hivi na viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii kama yanavyobainishwa na sheria za kitaifa na kimataifa bila kupindishwa pindishwa au kufumbiwa macho! Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba kuna zaidi ya watu milioni 46 waliotumbukizwa katika utumwa mamboleo sehemu  mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaofanyishwa kazi za suluba viwandani, migodini na mashambani kwa ujira “kiduchu”! Baadhi yao hasa wanawake wanajikuta wakitumbukia katika ndoa za shuruti, kazi za majumbani na biashara ya ngono!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na viongozi mbali mbali wa kidini dunia amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza mapambano dhidi ya utumwa mamboleo anaendelea kufafanua kwamba, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo mikutano ya wakuu wa dini pamoja na mameya wa miji mikuu duniani waliokutana na kuamua kujifunga kibwebwe ili kupambana na hatimaye, kung’oa kabisa utumwa mamboleo unaonyanyasa utu na heshima ya binadamu; matukio ambayo yamekuwa na umuhimu wa pekee kabisa katika mapambano haya.

Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, hivi karibuni alisikika akisema kwamba, kunako mwaka 2012 aliguswa kwa mara ya kwanza baada ya kusikia shuhuda za waathika wa biashara haramu ya binadamu, janga ambalo linazidi kupanuka kila kukicha. Viongozi wa kidini wamekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu kwa kuwasaidia waathirika katika mchakato wa kupambana na hali zao, kwa kuwarejeshea utu na heshima yao, tayari kuanza kuandika upya historia ya maisha yao! Ushirikiano kati ya Makanisa na vyombo vya ulinzi na usalama, vimesaidia sana katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu.

Kardinali Vincent Nichols anasema, ushirikiano huu ndio mwanzo wa kuanzishwa kwa “Kikundi cha Mtakatifu Martha” kunako mwaka 2014 kwa kupewa ushirikiano wa karibu sana na Baba Mtakatifu Francisko. Itakumbukwa kwamba, mwaka huo, Makamanda wakuu wa vikosi vya Jeshi la Polisi kutoka katika nchi 20 walikutanika pamoja, tukio ambao limeendelea kuwashirikisha viongozi wengine kutoka katika vyombo vya ulinzi na usama, sehemu mbali mbali za dunia. Utumwa mamboleo ni kashfa dhidi ya utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni kashfa inayogusa undani wa mwanadamu na kwa waamini wa Kanisa Katoliki ni kashfa inayotikisa Fumbo la Mwili wa Kristo.

Walimwengu wanapaswa kujifunza tena na tena anasema Baba Mtakatifu Francisko kusikitika kutokana na kuibuka kwa kasi kwa biashara ya utumwa mamboleo, ili waweze kuthubutu kufanya maamuzi magumu kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, janga kubwa katika ulimwengu mamboleo! Mashindano makubwa makubwa ya michezo kimataifa kama ilivyokuwa kwenye Michezo ya Olympic ya Mwaka 2012 huko Jijini London yamekuwa yakitumiwa na baadhi ya watu waliofilisika kimaadili na kiutu kuchochea biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kardinali Vincent Nichols anakaza kusema, mapambano dhidi ya utumwa mamboleo, yanapaswa kuwashirikisha watu katika medani mbali mbali za maisha bila kuwasahau watu wa kawaida, kwani hawa mara nyingi ndio wanaoshuhudia mara kwa mara matukio kama haya!

Ikumbukwe kwamba, utu na heshima ya binadamu vinafumbatwa katika kazi yake halali! Kumbe, kazi isiwe ni mahali pa kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu! Kazi ni jina, heshima na utumilifu wa utu wa binadamu! Kila mtu ajisikie kuwa nawajibika kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.