2018-02-06 16:51:00

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ukeketaji wa Wanawake na Wasichana


Tarehe 6 Februari 2018, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha  Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Ukeketaji wa Wanawake, na Watoto wa kike Duniani. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, yanapinga vikali ukeketaji dhidi ya wanawake.   Zaidi ya wanawake na wasichana milioni mia mbili wamekeketwa duniani, huku nusu yao wakiishi Misri, Ethiopia, Indonesia. Nchi za Somali, Guinea na Djibouti zikionyesha idadi kubwa ya wanawake waliokeketwa Barani Afrika. 

Wakati Dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya kumaliza kabisa vitendo vya ukeketaji na kufikia sifuri.  Umoja wa Mataifa unafanya kazi ya kuhakikisha kwamba mila hizi zinakoma mpaka kufikia mwaka 2030, mkakati uliotengwa kwenye Maendeleo endelevu ulio idhinishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa mwezi September, mwaka jana.  Kati ya watu milioni mia mbili waliokeketwa, Milioni 44 ni wasichana walio chini ya umri wa miaka 14  au wadogo zaidi ya hapo.  Katika nchi 30 duniani ambako vitendo hivi vinaendelea kutekelezwa, wasichana wengi  wamefanyiwa ukeketaji hata kufikia miaka mitano ya kusherehekea siku yao ya kuzaliwa.  Vitendo hivi ni wazi vinavunja Haki za Watoto.

UNICEF imesema kuwa kwenye nchi za Somalia, Guinea na Djibouti, mila ya ukeketaji ni kama imekubalika nchi nzima.  Vitendo hivi vimepungua sana katika nchi za Liberia, Burkina Faso, Kenya na Misri. Ambako hatua kubwa imepigwa kupinga mila hii.  Nchi tano zimepitisha sheria kali na kufanya vitendo vya ukeketaji  kuwa ni kosa la jinai.  Nchi hizoni pamoja na Kenya, Uganda na Guinea Bisau.   Na hivi karibuni nchi za Nigeria na Gambia pia zimepitisha sheria hiyo mwaka 2017. Msikilizaji, Wakati umefika wa kutokomeza kabisa ukeketaji kwa wanawake na wasichana duniani kote, kwa manufaa ya wote.  Kizazi chetu kiko kwenye hatari kubwa ni wajibu wa wote kufanya kila kinacho wezekana kwa mshikamano wa pamoja kupinga ukeketaji ili kuokoa kizazi kijacho, kwani Afya, Haki na Usawa wa mamilioni ya Wanawake na wasichana yanategemea umoja wetu katika kuiweka dunia iwe mahali pazuri na pema pa kuishi.  Basi kwa maelezo haya nimefikishwa mwishoni mwa ujumbe huu.

Pauline Mkondya,

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.