2018-02-05 09:27:00

Papa Francisko: Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai!


Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 4 Februari 2018, ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuadhimisha Siku ya 40 ya Maisha nchini Italia ambayo kwa mwaka huu imeongozwa na kauli mbiu “Injili ya maisha, furaha kwa walimwengu”. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatia shime Maaskofu pamoja na watu wote wenye mapenzi mema ndani na nje ya Italia, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ameonesha masikitiko yake kwa idadi ndogo ya wanachama wa utume wa familia waliojitokeza kwa ajili ya kulinda na kutetea Injili ya maisha, ikilinganishwa na miaka mingine iliyopita.

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia, kusimama kidete ili kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya maisha inayohatarishwa na biashara ya silaha duniani; sheria za utoaji mimba pamoja na utandawazi usiojali wala kuthamini utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali ili watu waweze kuamsha dhamiri nyofu ili kulinda Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika ujumbe wake kwa mwaka huu,unaojikita katika tafakari ya Neno la Mungu, linakaza kusema, “Injili ya maisha, ni furaha kwa walimwengu”. Ujumbe huu unachota amana na utajiri unaofumbatwa kwenye Wosia wake wa kitume uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ”Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” katika sura ya tano anakojikita zaidi katika upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Anasema, huu ni mchakato wa mwendelezo wa maisha ya binadamu na ukarimu wa kupokea zawadi ya maisha mapya ndani ya familia.

Kipindi cha mwanamke kubeba mimba ni muda wa ajabu sana hata kama wakati mwingine unakuwa na shida na changamoto zake. Huu ni wakati ambapo mwanamke anashirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya Uumbaji, kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu na kwamba, mtoto ana haki ya kuwa na baba na mama yake mzazi na hivyo kupata malezi na makuzi katika mazingira ya amani na utulivu. Baba Mtakatifu anawapongeza wanawake kwa mchango wao makini katika ustawi na maendeleo ya jamii pamoja na kuona mchango wa wanaume katika maisha na utume wa kifamilia.

Upendo wa kimama unaoneshwa pia katika kuasili mtoto na kwamba, ni kitendo cha upendo kutoa mtoto kwa familia ambayo haikubahatika kupata mtoto. Taratibu, sheria na kanuni maadili zinapaswa kuzingatiwa ili kuepuka tatizo la utoaji mimba na kutelekezwa kwa watoto baada ya kuasiliwa! Hapa familia zinahamasishwa kujenga utamaduni wa watu kukutana; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki, umoja, udugu; kwa kuwalinda na kuwasaidia wanajamii wanyonge sanjari na kushuhudia imani na matumaini ya kweli. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kupokea Ekaristi Takatifu kwa ukamilifu zaidi baada ya kutekeleza wajibu wao hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anawashauri watoto kuwapenda, kuwaheshimu na kuwasaidia wazazi wao. Amri hii inajikita katika heshima kwa watu wote. Wazee wanapaswa kutunzwa na kuhudumiwa kwa heshima, kwani wao wana mchango mkubwa katika kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii; hawa ni hazina ya historia ya jamii. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ujenzi wa udugu na kwamba, shule ni eneo muhimu sana katika ujenzi wa udugu, jamii na amani.  Wakwe nao waheshimiwe na kamwe wasibezwe anasema Baba Mtakatifu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linasema, njia pekee inayomwezesha mwamini kupata furaha ya maisha inafumbatwa katika upendo wa dhati, chimbuko na chemchemi ya maisha; furaha ya Injili inayoweza kushuhudiwa kwa walimwengu ni zawadi ya maisha ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu. Hii ni zawadi ambayo pia inafumbatwa katika Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, unaompatia dhamana na wajibu wa kutekeleza. Upya wa maisha na furaha inayofumbatwa katika upya huu, wanasema Maaskofu wa Italia ni neema inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kulindwa kwa kutambua kwamba, wao ni watoto wa Mungu wanaopaswa kufundwa katika upendo wa Mungu, daima kwa furahia zawadi ya maisha, kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu anayesimuliwa katika Injili!

Bwana Gian Luigi Gigli, Rais wa Chama cha Kutetea Maisha Italia, (MpV) anasema, “Injili ya maisha, furaha kwa walimwengu” inawezekana pale, tunu msingi za maisha ya Kiinjili zinamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu sanjari na kuendelea kujikita katika mchakato wa uponyaji wa madonda ya vitendo vya utoaji mimba na kifo laini, vinavyokumbatiwa na utamaduni wa kifo! Kuna haja ya kujenga na kudumisha upendo na mshikamano na wale wote wanaopambana na changamoto za maisha, ubinafsi na uchoyo, ili kulinda, kudumisha na kuenzi Injili ya maisha. Vitendo vya ghasia na mauaji vinahatarisha Injili ya maisha na hivyo kuwanyima walimwengu furaha, amani na utulivu wa ndani, badala ya kuufanya ulimwengu uwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.