2018-02-05 10:47:00

Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani kwa Mwaka 2018


Ugonjwa wa Saratani huanza pale seli za mwili zinapokuwa bila mpangilio na kusababisha kivimbe, na huweza kusambaa sehemu mbali mbali za mwili. Saratani huanza taratibu bila maumivu yeyote na huchukua muda kabla ya kuonesha dalili. Vitu vinavyochangia ukuaji wa saratani ni pamoja na virusi, bakteria, parasiti, madini mazito kwa mfano asbestos pamoja na mionzi. Dalili za sarani ni pamoja na kukosa hamu ya chakula, kupungua uzito bila sababu na uchovu bila kufanya kazi.

Uvimbe zaidi ya majuma matatu, matiti kubadilika maumbile, ngozi kukunjamana au chuchu kutoa maji maji au damu; mabadiliko katika kupata haja kubwa; kutokwa na damu katika haja kubwa na ndogo, puani au kwenye makohozi; kwenda haja ndogo mara kwa mara isivyo kawaida au mkojo kutoka kwa shida kubwa; mwanamke kutokwa na ute, maji maji, usaha au damu wakati wa kujamiiana, baada ya kukoma hedhi au nje ya mzunguko wa hedhi; maumivu wakati wa kula au kunywa; kukohoa au kuwa na sauti ya kukwaruza kwa zaidi ya wiki tatu. Saratani ikigundulika mapema inatibika kwa njia ya tiba mgando, upasuaji, dawa za sindano, dripu na tiba ya mionzi. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, mtu anawahi kituo cha afya ili kuchunguza afya yake.

Nchini Tanzania, tatizo la Saratani limekuwa likiongezeka kila mwaka. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa, kila mwaka wagonjwa wapya wapatao 50,000 hugundulika na saratani za aina mbalimbali Tanzania. Na kati ya hao ni wagonjwa 13,000 tu, sawa na 26% ndio wanaofanikiwa kufika katika Hospitali zetu kuweza kupata matibabu. Aidha, wagonjwa walio wengi (takribani asilimia 70) hufika Hospitalini kwa ajili ya matibabu wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa (hatua ya 3 na ya 4), hali ambayo hupunguza uwezekano wa wagonjwa kuweza kupona maradhi hayo.

Takwimu za mwaka 2016/2017 kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kwamba Saratani zinaoongoza nchini ni:

1. Saratani ya Kizazi ​(32.8%)

2. Matiti ​(12.9%)

3. Ngozi (Kaposis Sarcoma) ​(11.7%)

4. Kichwa na Shingo ​(7.6%)

5. Matezi ​(5.5%)

6. Damu ​(4.3%)

7. Kibofu cha Mkojo ​(3.2%)

8. Ngozi (Skin) ​(2.8%)

9. Macho ​(2.4%)

10. Tezi Dume ​(2.3%)

Katika kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani ninatoa wito na kuhimiza kila mmoja wetu kupima ugonjwa wa Saratani. Saratani inatibika endapo itagunduliwa mapema. Serikali ya Awamu ya 5 inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea na jitihada za kuongeza uelewa wa wananchi juu ya vyanzo mbalimbali vinavyosababisha saratani ili kila mmoja wetu aweze kujikinga. Vyanzo hivi ni pamoja na mtindo wa kimaisha (Life Style) kama vile uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula usiofaa (kula vyakula vyenye mafuta mengi, kutokula matunda na mboga mboga za kutosha), matumizi ya pombe kupita kiasi, matumizi ya dawa za kulevya na kutofanya mazoezi.

Aidha, Tutaongeza jitihada katika kuamsha ari na hamasa ya wananchi kupima Saratani ili kujua hali zao sambamba na kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya mabadiliko ya awali ya Saratani katika maeneo mbalimbali nchini hasa vijijini. Kwa mwaka 2017, Serikali imeongeza Vituo 100 kutoka vituo 343 vilivyopo awali kwa ajili ya huduma za kupima na matibabu ikiwa ni sehemu ya jitihada zetu za kupambana na ugonjwa huu. vituo hivi (Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali) tumevipatia vifaa tiba na utaalamu ili kuwezesha wanawake wengi kupima saratani ya kizazi na matiti pamoja na kupata matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya kizazi papo hapo. Tumelenga kuwafikia wanawake milioni 3 nchi nzima ifikapo Desemba 2018.

Vilevile, Serikali inaendelea na jitihada za kusogeza huduma za matibabu ya Saratani (matibabu kwa njia ya Dawa (Chemotherapy) na matibabu kwa njia ya mionzi (Radiotherapy) katika Hospitali zetu za Rufaa za Kanda (Mbeya, Bugando na KCMC). Pia tunaendelea kuimarisha huduma za matibabu ya Saratani katika Hospitali ya Ocean Road kwa kuweka mashine mbili mpya za kisasa (Linear accerelators), ambazo zitasaidia kupunguza muda wa kusubiri kwa wagonjwa kupata huduma za tiba ya mionzi sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100. Kuanzia mwezi April 2018, Serikali itaanza kutoa chanjo ya kuwakinga wasichana kupata ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi (HPV vaccine). Chanjo hii itatolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 - 14. Niwaombe wazazi na walezi wenzangu tuwe tayari kuhakikisha binti zetu wanapata chanjo hii. "Tunaweza, Ninaweza. Kwa Pamoja Tuwajibike Kupunguza Janga la Saratani Tanzania".!

Ummy Mwalimu, Mb

WAMJW

4 Februari 2018.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.