2018-02-03 16:01:00

Kamari ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha na utu wa binadamu


Michezo ya Kamari na Upatu ni donda ndugu linaloendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu mbali mbali nchini Italia. Kwa kutambua madhara makubwa ya michezo hii, kunako mwaka 1991 Padre Massimo Rastrelli alianzisha Mfuko wa kwanza nchini Italia, dhidi ya michezo ya kamari na upatu, kiasi cha changamoto hii kuvaliwa njuga na wadau sehemu mbali mbali za Italia. Lengo ni kujenga utamaduni wa kuwasikiliza na kuwasaidia waathirika wa michezo ya kamari na upatu; kwa kuwapatia elimu makini, sheria, kanuni na taratibu zinazoweza kuwakwamua kutoka katika hali hii sanjari na kuhakikisha kwamba, waathirika wanasaidiwa kujenga na kudumisha dhamiri nyofu, itakayowawezesha kutafuta kilicho chema, kizuri na kitakatifu katika maisha.

Katika kipindi cha miaka 26 Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II “Consulta Nazionale Antiusura, CNA,” imeweza kuzisaidia familia 25, 000 kwa kuokoa nyumba na vitega uchumi, kiasi hata cha kuweza tena kurejesha utu na heshima yao kama binadamu. Huu ni mchango mkubwa unaopaswa kuthaminiwa na kutambuliwa na wengi! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wa Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II, Jumamosi, tarehe 3 Februari 2018, walipokutana na kuzungumza naye mjini Vatican. Michezo ya kamari na upatu inadhalilisha na kuua; ni ugonjwa wa zamani sana, lakini bado unaendelea kuwadhalilisha watu wengi hata katika nyakati hizi.

Kumbe, kuna haja ya kujizatiti kikamilifu ili kuzuia na kuokoa maisha ya waathirika na vitega uchumi vyao; madeni makubwa ambayo mara nyingi wanashindwa kuyalipa kwa kuwapatia elimu ya kuwa na kiasi katika maisha pamoja na kujifunza kujinyima kwani kamwe mwanadamu hawezi kupata yote katika maisha. Watu waelimishwe umuhimu wa kuzingatia sheria pasi na shuruti, kujenga na kudumisha fadhila ya uaminifu, ukweli na uwazi katika maisha ya mtu binafsi na katika taasisi mbali mbali. Kuwepo na ongezeko la watu wa kujitolea ili kuwahudumia waathirika kwa kuwasikiliza, kuwashuri na kuwaongoza ili hatimaye, kuondokana na hali inayowanyanyasa na kuwatesa katika maisha, kiasi hata cha kuwanyima furaha, amani na utulivu wa ndani!

Myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa unatokana na ukweli kwamba, faida inapewa kipaumbele cha kwanza badala ya: utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu; kanuni maadili na utu wema; mshikamano na mafao ya wengi, lakini kumbe, haya ndiyo mambo ambayo yangepaswa kuzingatiwa katika sera na mikakati ya uchumi na maendeleo endelevu ya binadamu. Mchezo wa kamari na upatu ni matokeo ya myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kamari ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha ya watu na kudhalilisha utu wa binadamu na hivyo kuwa ni chachu ya rushwa, ufisadi na kizingiti katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Katika nchi ambamo kuna watu wengi wanaoteseka kutokana na umaskini wa hali na kipato; watu wanaoelemewa na madeni makubwa na waathirika wa makosa makubwa ya jinai pamoja na uwepo wa idadi kubwa ya wala rushwa na mafisadi, si rahisi sana kufanya mageuzi ya kiuchumi wala kuwa na uhakika wa usalama. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa michezo ya kamari na upatu ili kuokoa maisha ya watu wengi kama Kristo Yesu alivyofanya kwa kumtembelea Zakayo mtoza ushuru, akatubu na kumwongokea Mungu; Mathayo mtoza ushuru, akaacha yote na kuambatana na Kristo Yesu ili kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha.

Anawaombea viongozi wa serikali na taasisi za umma ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao, utakaowawezesha watu kufaidika na sheria, kanuni na taratibu za nchi kama ilivyo pia katika masuala ya kiuchumi! Mwenyezi Mungu awalinde na kuwasimamia wakuu na wafanyakazi wa vyombo vya fedha na mikopo ili waweze kuzingatia: sheria na kanuni; maadili na weledi kazini! Ikumbukwe kwamba, Benki nyingi duniani zimeanzishwa ili kupambana na umaskini, michezo ya kamari na upatu bila kutafuta faida kubwa.

Baba Mtakatifu anawashukuru kwa huduma inayojikita katika utamaduni wa kusikiliza, kujenga na kudumisha ujirani mwema, changamoto ni kumwangalia Kristo Yesu anayekutana na maskini, wagonjwa na viwete na kuwapatia tena uwezo wa kusimama na kusonga mbele na maisha yao! Mapambano dhidi ya michezo ya kamari na upati hayana budi kwenda sanjari na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ili kuwatangazia watu Injili ya matumaini kwa wale wote waliokata tamaa, ili kuweza kuzitegemeza familia na kwamba, fedha ni fedhea ya utu na heshima ya binadamu. Watu wajenge utamaduni wa kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kuwajibika pamoja na kuibua sera na mikakati itakayozuia athari za michezo ya kamari na upatu, daima mtu na familia wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu waliokolewa kutoka katika athari za michezo ya kamari na upatu ni mashuhuda wa Injili ya matumaini na huduma makini inayotolewa na Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II. Anawataka kuanza hija ya upendo na mshikamano na jirani zao pamoja na kuwatia shime wale ambao bado wanakandamizwa na athari za kamari na upatu kwamba, wanaweza kutoka huko na kuanza maisha mapya, ili kuanza ujenzi wa utu mpya wa kiuchumi dhidi ya uchumi, sera na mikakati inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.