2018-02-02 07:45:00

Uhuru wa kuabudu ni nguzo ya haki msingi za binadamu!


Utu na heshima ya binadamu; maana na misingi wa uhuru wa kidini; umuhimu wa mahusiano kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu; uhuru wa kidini unaofumbatwa katika maisha ya kijumuiya, kifamilia na mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ili kulinda na kukuza uhuru wa kuabudu, ni kati ya mambo muhimu sana yaliyochambuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusu “Dignitatis humanae” yaani “Uhuru wa kidini”.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walihimiza waamini kutenda kadiri ya imani yao, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo Yesu pamoja na Mitume wake katika huduma ya Injili ya upendo. Kanisa linapenda kuhimiza uhuru wa kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki katika hotuba yake elekezi katika kongamano lililokuwa linajadili kuhusu uhuru wa kidini na changamoto zake hasa Barani Ulaya, tukio ambalo liliandaliwa na Ubalozi wa Uingereza nchini Italia kutokana na uwepo wa Bwana Tariq Mahmood Ahmad, Baron Ahmad  Wimbledon, Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Uingereza Tukio hili limehudhuriwa pia na viongozi waandamizi kutoka Vatican.

Kardinali Leonardo Sandri, anasema, uhuru wa kidini ni jambo linalopaswa kusimamiwa na kutekelezwa na watu wote, kwa kutambua na kuthamini umuhimu wake katika maendeleo ya watu husika. Uhuru wa kidini unatoa utambulisho wa waamini na kwa Wakristo, uhuru wa kidini unawafanya kujitambua kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Amekumbushia kuhusu utume na huduma yake ya kidiplomasia aliyotoa huko nchini Mexico na kwa namna ya pekee, akamtaja Mtakatifu Josè Sanchez del Riò aliyeuwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani kunako mwaka 1928, matukio ambayo hata leo hii yanaendelea kujirudia sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Leonardo Sandri kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki amebahatika kutembelea huko Mashariki ya Kati na India ambako ameshuhudia umuhimu wa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali kuishi kwa pamoja katika umoja na udugu! Lakini pia kuna uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, kama vile uhuru wa kuabudu, hali inayoonesha uchungu na madonda makubwa katika maisha ya waamini wa Wakristo katika maeneo haya. Kuna wanawake na wasichana wanaolazimishwa kufunga ndoa za shuruti pasi na ridhaa yao wenyewe kama njia ya utekelezaji wa sera na mikakati ya wongofu wa shuruti. Uhuru wa kuabudu ni mapambano endelevu yanayopaswa kuvaliwa njuga na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na waamini wenyewe.

Tangu baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchakato wa uhuru wa kidini, lakini bado kuna mauaji, dhuluma, nyanyaso na ubaguzi dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia! Uhuru wa kuabudu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudi na uhuru wa kidini kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, kwani kuna baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaotaka kuzima uhuru wa kuabudu au kung’oa kabisa uhuru wa kidini kutoka katika masuala ya kisiasa na matokeo yake ni kuibuka kwa kasi kubwa chuki dhidi ya imani, dhuluma na nyanyaso. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuunganisha sauti zao ili kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu; kwa kujikita katika kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wajenge madaraja ya majadiliano ya kidini na kuheshimiana kama alivyofanya Padre Andrea Santoro aliyeuwawa kikatili huko Antiokia nchini Uturuki kunako tarehe 5 Februari 2006. Kanisa bado linamkumbuka kwa ushuhuda wake katika mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali nchini Uturuki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.