2018-02-02 14:28:00

Papa Francisko: Msitumie jina la Mungu kuhalalisha ghasia na maovu!


Utamaduni wa amani unafumbatwa na kusimikwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Hiki ni kiini cha hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Ijumaa, tarehe 2 Februari 2018 kwa wanasiasa na viongozi wa kidini, wanaokutana ili kujadili kwa pamoja changamoto zinazopelekea ghasia na mauaji kwa jina la Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa kupambana na changamoto hii inayoendelea kuenea kwa kasi ya ajabu sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja kwa viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanaondoa dhana inayohalalisha ghasia na mauaji kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwani kwa mwelekeo kama huu, unang’oa ukweli wa dini husika.

Viongozi wa kidini hawana budi kupinga vitendo vinavyokwenda kintume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu na mambo yote yanayotaka kuhalalisha matumizi ya nguvu kwa jina la Mwenyezi Mungu. Ghasia zinazofanywa kwa jina la dini hazina budi kukemelewa na kulaaniwa na wote, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni asili ya wema, upendo na huruma na wala ndani mwake, hakuna hata chembe ya chuki, hasira wala kulipiza kisasi. Waamini wanatambua kwamba, kufuru kubwa wanayoweza kuifanya ni pale wanapomweka Mwenyezi Mungu kuwa mtetezi wa dhambi, uhalifu na kumwita ili aweze kuhalalisha mauaji, mashambulizi, kuwatumbukiza watu katika utumwa na unyonyaji wa kila aina; dhuluma na nyanyaso kwa baadhi ya watu na hata wakati mwingine kwa jamii nzima.

Mwamini anapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu na hakuna mtu anayeweza kumtumia Mungu kwa ajili ya kutenda ubaya. Kila kiongozi wa kidini anahimizwa kuondokana na unafiki wa kumtumia Mwenyezi Mungu kwa mambo ambayo kamwe hayaendani la utukufu wake. Kuna haja ya kushuhudia bila ya kuchoka kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu, yanapaswa kulindwa, kuheshimiwa, kuhurumiwa pamoja na kudumisha mshikamano ili kuvuka dhana ya ukabila, udini, utamadani, itikadi au mwelekeo wa kisiasa. Kuwa mwamini wa dini yoyote ile hakumpatii mwamini huyo haki ya kuwatala au kuwanyanyasa wengine wasioamini katika dini yake.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa kisiasa, viongozi wa kidini, waalimu na wadau mbali mbali katika malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya bila kuwasahau wadau wa njia za mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni wadau wa utakatifu, utukufu na ukuu wa Mungu katika maisha yao. Mwelekeo huu utawasaidia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu anaye mkomboa mwanadamu kutoka katika hofu, chuki, ghasia na kwamba, anatamani kuwahudumia kwa kujikita katika fadhila ya ubunifu na nguvu ili kueneza na kudumisha mpango wake wa amani na upendo kwa watu wote. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, kwa hakika utamaduni wa amani unafumbatwa na kusimikwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili.

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.