2018-02-02 15:56:00

Padre Vedastus Mahinda ni "Jembe lililovunjika" mapema sana!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbu kumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili waweze kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Kifo kitakuja tu kwa wakati wake, kinaweza kuwahi au kuchelewa, lakini mwanadamu akumbuke kwamba, iko siku atakufa tu na hivyo kuungana na wahenga kwenye usingizi wa amani.

Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Familia ya Mungu nchini Tanzania inaomboleza kifo cha Padre Vedasto Mahimbi kutoka Jimbo Katoliki la Iringa, kilichotokea, tarehe 31 Januari 2018 kwa ajali ya gari eneo la njia panda ya Kilocha, Njombe.  Alikuwa akitoka Songea kuelekea Iringa. Tangu mwaka 2016 baada ya kuhitimu masomo yake ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, Roma, aliteuliwa kuwa Mhadhiri na Mwalimu wa Taaluma Seminari kuu ya Peramiho, Jimbo kuu la Songea. Taarifa kutoka Jimbo Katoliki Iringa zinaonesha kwamba, mazishi ya Marehemu Padre Vedasto Mahimbi yatafanyika Jumamosi, tarehe 3 Februari 2018 kwenye Makaburi ya Tosamaganga, Jimbo Katoliki la Iringa.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kufariki dunia, Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Padre Vedasto Mahimbi alikuwa ni “Jembe la falsafa” ambalo limekatika kabla ya wakati! Mnyenyekevu na mfano bora wa kuigwa na vijana! Anakumbukwa na wengi kama “Padre kutoka Tanzania”, mcheshi na mtu wa watu! Walimkubali kwa mahubiri yake Parokiani, kwani alitumia muda wake mwingi kuhakikisha kwamba, kweli Neno la Mungu linapikika ili liweze “kutafunwa na kumezwa hata na “vibogoyo”. Akiingia uwanjani kwa mpira wa kikapu, utadhani, huko ndiko alikobobea!

Anakumbukwa na watanzania wenzake waliobahatika kuishi na kusoma naye mjini Roma kwa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, hija ya kitume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa mwaka 2014 inafanikiwa! Haya ni machache kati ya mengi ambayo yamehifadhiwa katika nyoyo za watu ambayo, baadhi ya watu wanayakumbuka katika maisha na utume wa Marehemu Padre Vedasto Mahimbi, bila shaka Mama yake atamkosa sana hasa kwa ushauri kuhusu maisha na utume wa wanawake katika Kanisa mahalia, unaweza kufanya rejea ya vitabu vya mama yake mzazi bila shaka vinachapa na mkono wa Marehemu Vedasto Mahimbi! Jembe limetangulia, mipini inakuja nyuma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.