2018-02-01 14:00:00

Siku ya watawa duniani ni fursa ya kuomba Mungu zawadi ya miito!


Siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha siku ya Kutolewa Bwana Hekaluni, tarehe 2 Februari mwaka huu, inakwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya XXII Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani. Kwa maana hiyo,Kardinali João Braz de Aviz anawaalika wanachama wa Taasisi, mashirika na vyama vya kitawa wote kuudhuria katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican, yatakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko saa 11:30 jioni masaa ya Ulaya. Kardinali anasema, ni fursa na kuomba Mungu zawadi ya miito mipya ambayo iweze kupyaisha uso wa Kanisa na ulimwengu.

Kabla ya kilele cha siku hiyo, taarifa zinasema kuwa imetanguliwa na tukio la maombi ya sala na masifu ya jioni tarehe 27 Januari 2018, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane Laterano Roma yaliyoongozwa na Padre Antonio Panfili, Katibu Msaidizi wa Kitengo cha Mashirika ya Kitawa Jimbo la Roma,  . Taarifa ya Baraza la Kipapa  kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Vyama vya Kitume, inaandika kuwa, ni maelfu na maelfu ya watawa wa kiume na kike duniani kote ambao wanapokea zawadi ya wito kwa furaha na ukarimu wakiwa na karama mbalimbali, na kujikita katika kutafuta uso wa Bwana na katika kuwajibika kujenga amani na udugu japokuwa katika matatizo mengi.

Naye Kardinali João Braz de Aviz , Mwenyekiti wa Baraza hili anasema kuwa, kwa upande wao,wanahitaji kuhudumia mpango ambao ni kisima cha maisha ya kweli, chenye ukamilifu wa furaha na matumaini. Wao kama watawa, ni katika mwanzo wa uzoefu wa ubatizo, wameingizwa katika kisima cha maisha ya Mungu, familia na Kanisa, kwa maana hiyo ni warithi wa utajiri mkubwa wa wito na karama za Kanisa na wanahisi furaha na uwajibu wa kukitunza na kuhamasisha wito huo mtakatifu! Hivyo anathibitisha kuwa, maadhimisho hayo na Papa Francisko, ni muhimu kwa kwa maana ni sikukuu na wakati huohuo ni njia ya  kumshukuru Mungu na kusali kwa ajili ya kuomba zawadi ya miito ambayo inaweza kuendelea  kupyaisha uso wa Kanisa na katika dunia, na ili kutangaza furaha ya Injili na upendo wa Mungu anayetoa maana ya Maisha!

Sikukuu hii inatokana na nini?: Kwa mujibu wa utamaduni wa kiyahudi, kila mzaliwa wa kwanza wa kiume  alikuwa anapaswa awekewe wakfu kwa Bwana na ilikuwa ni sheria; wazazi wake walikuwa waende kutoa sadaka ekaluni , siku 40 baada ya kuzaliwa. Kulinga na utamaduni huo pia mwanamke alikuwa anafikiriwa kuwa damu yake haikuwa safi  mara baada ya kujifungua. Na iwapo alikuwa amejifungua mtoto wa kike, siku ziliongezwa hadi 66, lakini kwa upande wa mtoto wa kiume siku zilikuwa ni 40.  Katika kipindi cha Yesu, Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni na ile ya kutakasika kwa mama ikaangukia katika siku 40 baada ya kuzaliwa kwake Yesu, kwa mujibu wa Injili ya Mtakatifu Luka, akitoa ufafanuzi wa siku ya maadhimisho hayo. (Lk 2,22-24).

Hata hivyo zamani sana, sikukuu hiyo ilikuwa inaangukia tarehe 14 Februari, kwa maana ya kusema siku 40 baada ya Sikukuu ya tokeo la Bwana,  kwa kuelekezwa kama siku ya Mshumaa (Candelora) ikiwa ni sikukuu mila ya kipagani ya Lupercal nchini Italia mahali ambapo wao walikuwa wakifanya maandamano wakiwa na mienge ya moto. Hata hivyo katika kutazama ulinganifu wa sikukuu ya mila ya  kipagani na ile ya kikristo  ulikuwa haufanani tu katika kuwasha mishamaa, bali hata katika mawazo ya kutaka kutakasika. Katika suala la utakaso wa Mari na ule wa Yesu,  hata katika mila na tamaduni wa kipagani wa Lupercal jambo ambalo lilikuwa mstari wa mbele ni kutakasika, au baraka  kwa mishumaa au myenge ya moto ambayo ilukuwa inabarikiwa kwanza kabla ya kuanza maandamano.

Ni Papa Gelasio kati ya mwaka (492-496) ambaye aliomba na kupata  ruhusa kutoka Seneti ya Italia ili  kukomesha mila ya kipagani ya Lupercal, ambayo ilibadilishwa kabisa na  kuweka siku ya mishumaa ya Kikristo; Pia ni Papa  Justinian, katika karne ya sita(VI), aliye ondoa tarehe 14 Februari na kuanzisha tarehe 2 Februari, ikiwa ni siku ya 40 baada ya Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bwana! Kadiri siku zilivyoendelea mbele, siku ya mshumaa ikachukuliwa katika maadhimisho ya kiliturujia kwa mantiki ya Bikira Maria,wakionesha zaidi sura ya utakaso wa Maria kulingana na utamaduni wa mzaliwa wa kwanza, lakini wakati huu kwa mujibu wa ibada za kiliturujia, sikukuu hiyo niajikita kwa kina katika matazamo wa sura ya Kristo kwama  mzaliwa wa kwanza wa Mungu Baba!

Kwa kawaida baada ya maadhimisho ya misa ya sikukuu ya kutolewa kwa Bwana hekaluni, (Candlemas) waamini wengi hutunza mishumaa kama ishara ya ukombozi binafsi na majitoleo ya kikristo. Hiyo pia inajidhihirisha kabisa kwa maana maandhimisho hayo yanahitimisha siku inayofuata tarehe 3 Februari: Siku ambayo Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Mtakatifu Biagio. Katika maeneo mengi, wanahitimisha kwa baraka ya koo kwa kutumia mishumaa miwili iliyokuwa imebarikiwa siku moja kabla. Uthibitisho wa ishara hiyo unahusishwa na muujiza uliofanywa na Mtakatifu Biagio mara baada ya mtoto kupona baada ya kumeza mfuma wa samaki.

Sr Angela Rwezaula
Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.