2018-01-31 15:43:00

Jengeni utamaduni wa kuwasikiliza na kuwahusisha vijana katika utume


Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, nchini Italia, katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Siku kuu ya Mtakatifu Yohane Bosco, mwalimu wa vijana, ameitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Torino, kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana. Mtakatifu Yohane Bosco bado anaendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa vijana hata kwa nyakati hizi. Baba Mtakatifu Francisko alipotembea Jimbo kuu la Torino kunako mwaka 2015 aliitaka familia ya Mungu kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa vijana, kwa kuwa karibu sana na vijana ambao ni wadhaifu, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Hawa ndiyo wale wanaopaswa kupewa msukumo wa pekee katika mchakato wa uinjilishaji wa kina!

Kwa kutambua na kuthamini maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, Askofu mkuu Cesare Nosiglia, ameandika Barua ya Kichungaji kwa mwaka 2017-2018 kwa ajili ya vijana na walezi wao, inayoongozwa na kauli mbiu “Mwalimu, una kaa wapi?” Ni barua inayojikita kwa namna ya pekee katika maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ambayo imeitishwa na Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni mwendelezo wa majiundo endelevu wa familia ya Mungu, Jimbo kuu la Torino, ambalo kwa miaka ya hivi karibuni imejikita zaidi katika kukuza na kudumisha mahusiano kati ya vijana wa kizazi kipya na “wahenga”.

Barua hii ni mwongozo, taratibu na dira kwa maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa Jimbo kuu la Torino. Lengo ni kukazia majiundo ya awali na endelevu katika maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kitaaluma, ili kuwajenga na kuwafunda vijana wanaoweza kupambana na changamoto kutoka katika medani mbali mbali za maisha, na wakabaki salama na thabiti katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Maisha na shughuli mbali mbali zinazofanywa kwa ajili ya vijana zinapaswa kuwa ni sehemu ya majiundo yao ndani ya Kanisa, ambamo wamezaliwa kwa “Maji na Roho Mtakatifu”; mahali ambamo, wanaendelea kulishwa kwa Neno la Sakramenti za Kanisa, tayari kumshuhudia Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku kama kielelezo cha imani tendaji!

Askofu mkuu Cesare Nosiglia, anasema, vijana wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na upendo, kwa kujali mahitaji yao: kiroho na kimwili; ili waweze kukuza na kudumisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana waoneshwe upendo ambao pengine wanaukosa kutoka katika familia na jamii inayowazunguka! Vijana wajengewe utamaduni wa ukarimu, upendo na mshikamano na jirani zao; wawe makini katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, daima kwa kutafuta kilicho chema, cha kweli na kitakatifu.

Vijana wafundwe kuishi na kuimwilisha Injili katika uhalisia wa maisha yao, kwa njia ya ushuhuda unaotolewa na familia ya Mungu katika ujumla wake. Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha sera na mikakati kwa ajili ya utume kwa vijana wa kizazi kipya: kwenye familia, shule na maeneo ya kazi na michezo. Kila mahali iwe ni fursa ya kurithisha imani kwa vijana wa kizazi kipya, dhamana inayopaswa kutekelezwa na familia, parokia na familia ya Mungu katika ujumla wake. Vijana wasaidiwe kuwa wahusika wa mabadiliko na mageuzi yao wenyewe, washiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu, daima mshikamano wa huruma na upendo, vikipewa msukumo wa pekee. Kuanzia tarehe 11-12 Agosti, 2018, vijana kutoka Torino watamtembelea Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, ili aweze kuwamegea Injili ya furaha na matumaini katika hija ya maisha yao. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Torino, iwajibike barabara katika kukuza na kudumisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa, tema itakayopembuliwa kwa kina na mapana wakati wa maadhimisho ya baraza kuu la kichungaji, Jimbo kuu la Torino, Mwezi Juni, 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.