2018-01-31 07:45:00

Askofu mkuu Scicluna atumwa Chile kuchunguza kashfa ya nyanyaso!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni mara baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Chile iliyokuwa ikiongozwa na kauli mbiu “Amani yangu nawapeni” alisema, kwa ujumla, hija yake ilikuwa na mafanikio makubwa licha ya maandamano na vurugu zilizojitokeza kabla na wakati wa hija yake ya kitume, kiasi cha Makanisa kadhaa kuchomwa moto! Baba Mtakatifu alisikitika kusema, kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini Chile zimechafua maisha na utume wa Kanisa na kwamba, alichukua fursa ya hija yake ya kitume, kuomba msamaha kwa wale wote waliotikiswa na kuguswa na kashfa hii!

Kashfa hii ilichafua ukurasa wa hija ya Baba Mtakatifu nchini Chile alipoonekana kana kwamba, alikuwa anamtetea Askofu Juan de la Cruz Barros Madrid, wa Jimbo Katoliki Osorno nchini Chile, kwa kutaka ushahidi ili aweze kumwajibisha Askofu wa Osorno dhidi ya shutuma zilizokuwa zinamwandama! Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzingatia utete wa tatizo hili kimaadili “Delicta graviora”, ameamua kumtuma Askofu mkuu Charles J. Scicluna, wa Jimbo kuu la Malta kwenda nchini Chile ili kusikiliza shutuma na kukusanya ushahidi, ili hatimaye, kesi hii iweze kujadiliwa kwenye Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na maamuzi kuchukuliwa kwa kuzingatia ukweli, uwazi na haki kwa wale wote wanaohusika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.