2018-01-30 06:39:00

Papa Francisko: Epukeni kirusi cha kutowajali wengine ni hatari sana!


Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo Barani Ulaya, OSCE, chini ya uongozi wa zamu kutoka Italia, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wajibu wa Serikali, Taasisi na Watu Binafsi katika mapambano ya dhuluma na chuki dhidi ya Wayahudi” Jumatatu, tarehe 29 Januari 2018 limefanya mkutano wake kwa kukazia haki msingi za binadamu, dhidi ya sera za ubaguzi wa rangi, hofu isiyokuwa na msingi na ubaguzi, ili kujikita zaidi katika maridhiano kati ya watu pamoja na mapambano dhidi ya ubaguzi wanaofanyiwa Wakristo pamoja na waamini wengine duniani! Shirikisho la OSCE linayajumuisha mataifa 57 kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Wajumbe, wa mkutano huu, wamepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko amekazia wajibu ili kufanya upembuzi yakinifu mintarafu sababu msingi zinazopelekea ghasia na vitendo vya kibaguzi pamoja na hali ya kutojali shida na mahangaiko ya wengine, kiasi cha baadhi ya watu kushindwa kutenda haki hata kama wanatambua umuhimu wa haki katika jamii. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuachana na virusi vya ubaguzi unaofumbatwa katika utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kwa kutambua kwamba, kimsingi mwanadamu ni kiumbe jamii na kwamba, dhana ya amani, utulivu na usalama ni mchango na wajibu wa watu wote.  

Mzizi wa kifo unapelekea watu kushindwa kuthaminiana na matokeo yake ni ukimya unaofumbata kifo kama ilivyokuwa kwenye kambi za mateso huko Auschwitz-Birkenau. Huu ni ukimya unaomwachia mtu machozi na majonzi moyoni, sala na mchakato wa kuomba msamaha. Ili kupambana na virusi hivi, Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kujenga kumbu kumbu endelevu, kwa kufanya rejea na kujikita katika mambo msingi ambayo yamekuwa ni sehemu ya hija ya maisha ya binadamu, ili kuokoa tena utu na heshima ya binadamu na hatimaye, kuondokana na chuki pamoja na uhasama unaoweza kuoneshwa kwa jirani. Kumbu kumbu endelevu ni mchakato unaowaunganisha watu wote, ili kuwa na mwelekeo wa kesho iliyo bora zaidi, dhamana inayopaswa kufundishwa kwa vijana wa kizazi kipya!

Hati ya tunakumbuka: tafakari kuhusu Shoah, iliyotolewa kunako mwaka 1998, inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu ilipochapishwa kwa kukazia kumbu kumbu endelevu inayopaswa kudumishwa kwa kuungana na Wayahudi, ili kamwe kusitokee tena mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi. Hakuna kesho iliyo bora zaidi pasi na kumbu kumbu endelevu! Ili kuandika historia, kuna haja ya kuwa na kumbu kumbu ya pamoja ambayo ni hai na inayosimikwa katika imani na matumaini, licha ya changamoto zilizopo. Kanisa linapenda kuanzisha mchakato wa waamini kutembea kwa pamoja likikumbuka ule urithi ulio wa umoja na Wayahudi, na likisukumwa na visa visivyo vya kisiasa, bali vya kidini, yaani upendo wa Kiinjili, lina shutumu chuki na udhalimu na aina zozote za ukatili dhidi ya Wayahudi wakati wowote na kwa yeyote yule! Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kujikita katika mawasiliano na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya dhidi ya udhalimu, chuki na ubaguzi, ili hatimaye, kusahau yaliyopita na kuanza kuganga yaliyopo na yale yajayo! Binadamu wajifunze kutafuta kilicho kizuri na kukiambata kwa pamoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.