2018-01-27 13:29:00

Siku ya Ukoma Duniani kwa Mwaka 2018: Pambaneni na maambukizi mapya!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu katika maadhimisho ya Siku ya 65 ya Ugonjwa wa Ukoma Duniani kwa Mwaka 2018 anasema, maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukoma ni hatari kwa utu na heshima ya binadamu, kwani, wengi wao wanabaguliwa, wanatengwa na kunyanyapaliwa na jamii. Wadau mbali mbali kwa kushirikiana na Mfuko wa Afya wa Sasakawa kutoka Japan, Jeshi la Malta, Mfuko wa Raoul Follereau pamoja na Mfuko wa Msamaria mwema, wanaendelea kuhimiza umuhimu wa viongozi wa kidini kusaidia kuelimisha umma dhidi ya tatizo la kuwabagua na kuwanyanyapalia wagonjwa wa Ukoma duniani.

Shirika la Afya Duniani linasema, imani potofu kama vile kulogwa zimeripotiwa kuwa ni kikwazo katika kutibu ugonjwa wa Ukoma wakati huu ambapo maambukizi mapya 200,000 ya ukoma huripotiwa kila mwaka.  Umoja wa Mataifa unazitaka nchi wanachama kuhakikisha kwamba, linauvalia njuga ugonjwa wa Ukoma pamoja na kupambana na vitendo vya unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa Ukoma. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015 kumekuwepo na maambukizi mapya ya Ukoma 212, 000 sehemu mbali mbali za dunia, lakini asilimia 60% ya waathirika wote walikuwa wanatoka nchini India. Nchi nyingine ni Brazil na Indonesia. Takwimu zinaonesha kwamba, watoto walioambukizwa Ukoma ni asilimia 8.9% ya wagonjwa wote duniani na kwamba, asilimia 6.7 ya watoto wagonjwa walionesha mabaka mwilini wao!

Imegota miaka 65 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Ukoma Duniani toka mwaka 1954, Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hiyo huku kaulimbiu ikiwa ni “tokomeza ulemavu unaotokana na ukoma miongoni mwa vijana”. Akiongea na vyombo vya habari makao makuu ya Wizara ya afya kwa niaba ya Waziri mkuu wa Tanzania, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa, katika maadhimisho haya lengo lake ni kuikumbusha jamii na kuielimisha juu ya ugonjwa wa ukoma na kuongeza kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya maeneo nchini Tanzania 

Akitaja maeneo ambayo bado yana changamoto ya ukoma, Ndugulile amesema kuwa kuna mikoa 10 ambayo inagundua wagonjwa wapya kila mwaka ambayo ni Lindi, Rukwa, Mtwara, Morogoro, Pwani, Tanga, Geita, Dodoma, Tabora na kigoma. Lakini pia amezitaja wilaya 20 ambazo kiwango cha ukoma kipo juu sana na bado hazijafikia lengo la utokomezaji ambazo ni Liwale, Nkasi, Ruangwa, Nanyumbu, Shinyanga manispaa, Kilombero, Mafia, Pangani, Mvomero, Masasi mjini, Lindi vijijini, Kilwa, Mpanda, Nachingwea, Rufiji, Korogwe, Mkinga, Ulanga, Morogoro vijijini na Chato.

Sambamba na hayo Naibu Waziri amezitaja dalili za awali za ugonjwa wa ukoma ambazo ni kutokwa mabaka kwenye ngozi yenye rangi ya shaba na hayawashi wala kuuma na pia mabaka haya hukosa hisia ya joto, mguso au maumivu na kuongeza kuwa dalili nyingine za ukoma ni pamoja na vijinundu kwenye ngozi hasa usoni au masikioni na uvimbe na maumivu kwenye mifupa ya fahamu. Pia Naibu Waziri Ndugulile ameeleza mipango ya serikali katika kutokomeza kabisa ugonjwa huo ambao hutokana na vimelea vya ukoma viitwavyo “Myco-Bacteria Leprae” na kusema kuwa serikali imechukua hatua ya kuendesha kampeni ya ugunduaji wa wagonjwa wapya kwa kila kijiji ndani ya halmashauri zinazoongoza nchini Tanzania.

Serikali ya Tanzania imejipanga kuendesha zoezi la kutoa kinga katika ngazi ya kaya sambamba na kuagiza na kusambaza dawa za kutosha za ukoma nchini kote. Aidha Naibu Waziri amewahasa wagonjwa wote pamoja na jamii inayowazunguka kujitokeza ili kuweza kupata matibabu yanayostahili na kuachana na mila potofu huku akisisitiza kuwa ugonjwa wa ukoma siyo ugonjwa wa kurogwa na kuongeza kwamba, matibabu ya ukoma hutolewa bure kabisa katika vituo vyote vya afya hapa nchini. Mwisho kabisa Naibu Waziri ameiomba jamii kujenga tabia ya kuchunguza miili yao mara kwa mara ili kuweza kuuzuia ugonjwa wa Ukoma ukiwa katika hatua ya awali jambo ambalo litasaidia pia kupunguza kusambaa kwa ugonjwa huo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.