2018-01-24 13:15:00

Papa Francisko: Hata Wanajumuiya ya Yazidi wanayo haki ya kuabudu!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya katekesi yake, Jumatano, tarehe 24 Januari, 2018 amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa Jumuiya ya Yazidi kutoka Ujerumani, ili kuwaonesha mshikamano wake, lakini zaidi na wale wanaoishi nchini Iraq na Siria ambako wanakabiliana na vitendo vya kinyama na mashambulizi ya mara kwa mara, jambo ambalo anasema Baba Mtakatifu kamwe haliwezi kukubalika. Hawa ni watu wanaouwawa kutokana na imani yao. Kila mtu anayo haki ya kuungama na kumwilisha imani yake katika matendo bila ya kipingamizi chochote.

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Yazidi ina utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kitamaduni, lakini kwa miaka ya hivi karibuni imejikuta ikiogelea katika dimbwi la uvunjwaji wa haki msingi za binadamu; kwa kutekwa nyara, kutumbukizwa utumwani, kuteswa na wongofu wa shuruti kuuwawa kikatili. Maeneo ya hija na ibada anasema Baba Mtakatifu yameharibiwa sana na vita, wale waliobahatika waliweza kukimbilia ughaibuni ili kuokoa maisha yao, hali ambayo imewafanya kuacha mambo msingi na matakatifu nyuma yao.

Hadi leo hii, kuna makundi madogo madogo ya waamini wanao teseka sehemu mbali mbali za dunia kati yao kuna wakristo wanaoteseka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Vatican itaendelea kupaaza sauti ili kutetea makundi ya namna hii, ili yaweze kutambuliwa, kulindwa na kuheshimiwa. Vatican inataka kukuza na kudumisha majadiliano, upatanisho ili hatimaye, kuganga na kuponya madonda yote yanayowaandama! Haya ni matunda ya nguvu za giza zinazomwandama mwanadamu, kiasi cha kumwona jirani na ndugu yake kuwa ni adui na mbaya wake, hali inayomwondolea mtu utu na heshima yake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa mara nyingine, anapenda kupaaza sauti yake ili kutetea haki msingi ya Jumuiya ya Yazidi kuendelea kuwepo kama Jumuiya ya kidini kwani hakuna mtu mwenye dhamana ya kufuta dini ya mtu. 

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wanajumuiya ya Yazidi ambao hadi sasa wako mikononi mwa wateka nyara na magaidi. Anawaombea ili waweze kupata ujasiri wa kuwatafuta ndugu, jamaa na rafiki zao aliotangulia mbele za haki ili waweze kuwapatia maziko wanayostahili. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwajibikika kusikiliza  na kujibu kilio cha mateso na mahangaiko ya wanajumuiya ya Yazidi. Anawaalika watu wenye mapenzi mema kusaidia ujenzi wa makazi na nyumba za Ibada sanjari na kuendelea kuboresha mazingira yatakayowawezesha wakimbizi na wahamiaji kurejea tena nchini mwao, huku Jumuiya ya Yazidi ikihifadhi kumbu kumbu ya utambulisho wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu kuwasaidia ili kweli waweze kuwa ni wajenzi wa ulimwengu ambamo watu wanaweza kuishi kwa amani na udugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.