2018-01-22 14:41:00

Papa Francisko: Sala ya kimissionari inawaunganisha watu wa Mungu


Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù, Jumapili tarehe 21 Januari 2018 ameianza kwa Masifu ya Adhuhuri kwa kusali na watawa wa ndani, kwenye Madhabahu ya “Senor de los Milagros” yaani “Bwana wa Miujiza” na kuhudhuriwa na watawa zaidi ya 500.  Hili ni eneo ambalo ni maarufu sana kwa waamini nchini Perù, wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya sala. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amesema, amependa kuungana nao ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na utajiri wa zawadi mbali mbali za maisha ya Kikristo pamoja na kuwa na furaha ya kutambua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu.

Hili ni jibu makini mintarafu upendo wa Mungu kwa binadamu, mwaliko kwa watawa ni kuhakikisha kwamba, kila siku ya maisha yao, wanajitahidi kupyaisha furaha hii inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Mambo msingi wanayopaswa kuzingatia katika safari ya maisha na wito wao ni: maisha ya sala binafsi na zile za kijumuiya, kiini cha maisha ya watawa wa ndani. Ni fursa ya kukuza na kudumisha mang’amuzi ya upendo wa Mungu unaobeba na kufumbata imani na hivyo kuifanya sala kuwa ni chimbuko la umissionari.

Sala ya Kimissionari inawaunganisha waamini wote wanaotekeleza dhamana na wajibu wao sehemu mbali mbali za dunia, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia upendo na matumaini, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili. Ni nguvu inayowawezesha hata mashuhuda wa imani kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Upendo ni mhimili wa daima kwa miito yote ndani ya Kanisa. Upendo wa Mungu unaokoa na kufariji. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Sala ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Anawahimiza watawa wa ndani kusali kwa ajili ya kuwaombea wafungwa, wahamiaji, wakimbizi, wanaoteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; kwa familia zinazoogelea katika kinzani na mipasuko.

Watawa wawakumbuke na kuwasindikiza watu wasiokuwa na fursa za ajira, maskini na wagonjwa, bila kuwasahau waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya. Watawa  wa ndani katika maisha na utume wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.  Wao ni wawakilishi wa mateso, mahangaiko na matumaini ya familia ya Mungu, ili kupata neema na hatimaye, kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. kwa njia ya sala zao, watawa wanaweza kusaidia kuganga na kuponya madonda ya waamini wengi.

Maisha ya watawa wa ndani, si gereza linalowanyima watu uhuru, bali ni eneo ambalo linadumisha mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa na Kristo Yesu, kiasi cha kuwajalia neema ya kusikiliza upya mateso na mahangaiko ya watu; hali ya watu kuchanganyikiwa na kukata tamaa pamoja na changamoto zinazowakabili watu wengi wanaopambana na utamaduni wa kutowajali wengine unaotawala kwa nyakati hizi. Sala kwa ajili ya kuombea mahitaji mbali mbali ya watu wa Mungu inapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya sala kwa watawa wa ndani na pale inapowezekana, sala hizi zimwilishwe katika huduma ya upendo.

Baba Mtakatifu anawataka watawa wa ndani kuendeleza ile Sala ya Kikuhani ya Kristo Yesu, aliyesali na kuomba ili wote wawe na umoja, kama jinsi wao katika Fumbo la Utatu Mtakatifu walivyo wamoja, ili ulimwengu upate kusadiki. Waendelee kusali kwa ajili ya umoja wa Kanisa; Umoja katika imani, matumaini na mapendo. Huu ni umoja unaowaunganisha wote katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kiasi hata cha kuweza kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi ni Fumbo kuu la Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka watawa wa ndani kusali zaidi kwa ajili ya umoja wa Kanisa nchini Perù.

Baba Mtakatifu anawataka watawa waendelee kujizatiti katika ujenzi wa umoja na udugu ili wawe ni mwanga unaofukuzia mbali matendo ya utengano na kinzani kwa kutangaza na kushuhudia kwamba, umoja na udugu ni jambo linalowezekana katika maisha ya kitawa. Watawa wawe ni mashuhuda wa upendo wa kidugu unaotafutwa kwa udi na uvumba katika ulimwengu mamboleo. Watawa wahakikishe kwamba, wanajitahidi kuishi wito wao kwa uaminifu unaotangaza na kushuhudia upendo wa Mungu. Daima Kristo Yesu, awe ni kiongozi wao mkuu, kwani Kristo mwenyewe anasema ni: Njia, Ukweli na Uzima. Watawa wa ndani watambue kwamba, Mama Kanisa anawahitaji na kuwathamini sana. Wao ni mwanga unaomwangazia Kristo Yesu, ambaye ni: Njia, Ukweli na Uzima, anayemkirimia mwanadamu maisha tele na utumilifu wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaomba watawa wa ndani kusali kwa ajili ya Kanisa na viongozi wake; kwa ajili ya watawa na familia mbali mbali; kwa ajili ya wagonjwa, watenda dhambi na wale wanaowanyanyasa ndugu na jirani zao. Amewaomba kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.