2018-01-21 15:41:00

Papa Francisko akutana na wanafunzi wa Taasisi ya Kipapa Kimataifa!


Wanafunzi wa Taasisi ya Kipapa ya“Scholas Occurentes”  iliyoanzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 inawataka vijana wa kizazi kipya kugundua maana ya maisha, ili waweze kuyasherehekea, kwani ujana ni mali, fainali iko uzeeeni! Vijana waonje uzuri na utakatifu wa maisha, ili kuyaadhimisha kikamilifu, licha ya matatizo na changamoto mbali mbali zinazomzunguka mwanadamu kwa kutopea kwenye utamaduni wa kifo. Shule ni mahali muafaka pa kuwafunda vijana maana ya maisha, kwa kujiweka wazi kwa wale wasiowafahamu, ili kuchanganyika na hatimaye, kufutilia mbali kabisa maamuzi mbele ambayo yamekuwa ni chanzo cha kinzani na mikwaruzo miongoni mwa jamii mbali mbali za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wazazi na walezi kuwapatia vijana wa kizazi kipya, fursa ya kuwa na ndoto ya kucheza, ili kujenga moyo wa shukrani na hatimaye, kukuza kipaji cha ubunifu kitakachowasaidia vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii wanamoishi! Wazazi na wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini ili kuibua, kushuhudia na kutangaza Injili ya matumaini inayofumbatwa katika sakafu ya maisha ya vijana, ili hatimaye, ndoto yao iweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya vijana wa kizazi kipya.  Shule pawe ni mahali pa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana; kushikamana katika umoja na kuthamini tofauti msingi zilizopo, ili kufikia usawa bila ya kulazimika wote kuwa sawa sawa, kwani udugu si kufanana bali ni kusaidiana. Hiki ndicho kilio cha walimwengu wa nyakati hizi.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamoi, tarehe 20 Januari 2018 wakati wa hija ya kitume chini Perù, amekutana na kuzungumza kwa faragha na kikundi cha wanafunzi 200 kutoka katika Taasisi ya Kipapa ya “Scholas Occurentes” kutoka shule 34 zinazomilikiwa na kuendeshwa na serikali, watu binafsi na mashirika ya kidini nchini Perù. Baba Mtakatifu pamoja na wanafunzi hawa wamezungumzia changamoto wanazokutana nazo vijana katika safari ya maisha yao na miradi ambayo wangependa kuiendeleza kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya miji yao. Wanafunzi wa Taasisi hii wameweza kufanikisha ndoto hii kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu pamoja na msaada wa kifedha kutoka Benki ya Maendeleo Amerika ya Kusini, IDB.

Wanafunzi wameweza kufanya tafiti na kuchunguza athari mbali mbali katika maisha, ili hatimaye, waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya maisha ya vijana wenzao. Vijana wemejifuza umuhimu wa uzalendo na uraia; ubaguzi na ubinafsi unaomong’onyoa mafungamano ya kijamii. Mkusanyiko wa wanafunzi wa Taasisi ya Kipapa ya “Scholas Occurentes” kutoka shule 34 nchini Perù umehitimishwa na Bwana Josè Maria del Corral, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya “Scholas Occurentes” kimataifa. Wanafunzi hawa wamejikita katika katika mchakato wa kudumisha amani, umoja na matumaini miongoni mwa wanafunzi wenzao, tukio ambalo limemgusa kwa namna ya pekee kabisa Askofu mkuu Josè Luis Palacio Perez Medel. Vijana wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko anaye endelea kulihamasisha Kanisa kuwekeza, kuwasindikiza na kuwasikiliza vijana ili kujibu matamanio yao halali na matunda ya kazi hii, yataonekana kwa wakati wake. Wanafunzi hawa wamemshirikisha Baba Mtakatifu fursa, changamoto, matatizo na matamanio yao kwa siku za usoni. Taasisi ya Kipapa ya “Scholas Occurentes” itaendeleza dhamana na majukumu yake, hata mara baada ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù, baada ya kuwekeana sahihi makubaliano kati ya Taasisi hii ya Kipapa na Serikali ya Perù, kwani wanafunzi wameonesha ujasiri, unyenyekevu na ukomavu mkubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.