2018-01-20 11:54:00

Papa Francisko: Watoto wanahitaji mashuhuda wa Injili ya matumaini


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kutembelea na kuzungumza na watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, wanaohudumiwa kwenye  Kituo cha Jorge Basadre, huko Puerto Maldonado, nchini Perù, Ijumaa, tarehe 19 Januari 2018 amepata nafasi pia ya kutembelea Kituo cha “Hogar Principito” yaani “Nyumba ya Mfalme Mdogo”. Hii ni nyumba inayotoa hifadhi kwa watoto 40 wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi na ilizinduliwa kunako mwaka 1996 na Padre Xavier Arbex de Morsier.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kurejea tena katika Fumbo la Umwilisho lililotoa nafasi ya pekee, kwa Mama Kanisa kutafakari kuhusu utu, heshima na hatima ya watoto wadogo ambao wanapaswa kuwa ni amana na utajiri wa familia na jamii katika ujumla wake. Amesikitika kusema kwamba, wakati mwingine, watu wazima hawatoi kipaumbele cha pekee kwa maisha, ustawi na maendeleo ya watoto katika jamii. Hawa ni watoto ambao wanakosa uwepo wa wazazi na walezi wao, lakini uwepo wa Baba Mtakatifu kati yao ni mwanga wa matumaini kwa watoto wote wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi! Huduma inayotolewa Kituoni hapo inawasaidia kugundua uso wa Mungu anayewalinda na kuwasimamia, kiasi cha kujaza Injili ya upendo katika mazingira ya Kituo hiki na rasimali kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Watoto wanahitaji kuwa na mifano bora ya kuigwa, kumbe hata watoto hawa wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa mwanga wa matumaini kwa watoto wenzao wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi! Ikumbukwe kwamba, misitu ni rasilimali na utajiri wa watu mahalia kwani katika misitu, watu wanajipatia chakula na dawa; lakini inasikitisha kuona jinsi ambavyo mazingira na vyanzo vya maji vinavyochafuliwa na matokeo yake ni vifo vya watu! Baba Mtakatifu anawaambia watoto hawa kwamba, wanayo fursa ya kusoma na kujiandalia maisha kwa kesho iliyo bora zaidi, basi wahakikishe kwamba, wanaitumia nafasi hii kikamilifu. Wajitahidi kutafuta asili ya maisha yao, wajenge utamaduni wa kuwasikiliza wahenga na kuthamini mila na desturi zao njema! Vijana wasimame kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wadau wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kuganga na kuponya madonda ya watoto hawa kutoka Amazonia kwa mafuta ya huruma na upendo wa Mungu, ili hatimaye, waweze kuwa ni wadau katika ujenzi wa jamii na ulimwengu katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.