2018-01-20 11:29:00

Papa Francisko: Perù inapaswa kujizatiti kupambana na utumwa mamboleo


Utamaduni wa watu kutoka sehemu mbali mbali za Perù kuweza kukutana kunajenga na kupyaisha Injili ya maisha inayofumbatwa katika Injili ya matumaini kwa watu wa Mungu. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 19 Januari 2018 wakati alipokutana na kuzungumza na watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, wanaotunzwa kwenye Kituo cha Jorge Basadre, huko Puerto Maldonado, wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù.

Watoto katika ushuhuda wao, wamemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuthubutu kuwatembelea na kuwajulia hali katika eneo hili ambalo limejeruhiwa sana kutokana na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu kiasi hata cha kuonekana kana kwamba, limesahauliwa na kutelekezwa! Baba Mtakatifu amewakumbusha watoto hawa kwamba, wao wanaishi katika eneo ambalo ni urithi kutoka kwa wahenga wao. Bikira Maria, Mama wa Mungu katika maisha na utume wake, alipambana na mazingira magumu na hatarishi, kiasi hata cha kuthubutu kuishi ugenini ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu! Bikira Maria katika maisha na unyenyekevu wake, akawa kweli ni chemchemi ya Injili ya furaha inayofunuliwa kwa wale walio wadogo na wanyenyekevu wa moyo!

Baba Mtakatifu amewaambia watoto hawa kwamba, kwao Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa na Mama anayewapenda na kuwaombea; na kamwe wasijisikie pweke na yatima, kwani wanaweza kuonja furaha ya Injili kutokana na familia na jumuiya inayowatunza, kiasi hata cha kuwawezesha kuwa na nguvu ya kuweza kupambana na changamoto za maisha, hata kama hawawezi kuzitatua zote katika ujumla wake. Baba Mtakatifu amekemea sana tabia ya baadhi ya watu kutaka kulifanya eneo hili kuwa ni ardhi kavu na kame isiyoweza kuzalisha chochote, lakini Habari Njema ni kwamba, wote ni watoto wa Mungu anayewawezesha  kutambuana kama ndugu.

Utamaduni usiojali mahangaiko ya watu una tabia ya ubaguzi kiasi hata cha kutaka kuwafumba watu midomo, ili washindwe kuona na kusimamia haki zao msingi, ili kuwatumbukiza katika janga la ulaji wa kupindukia, bila kuguswa hata kidogo na mateso ya jirani zao. Huu ni utamaduni usiokuwa na mvuto wala mashiko; hauna  mafungamano wala sura. Ni utamaduni usiokuwa na mama unaopania ulaji wa kupindukia. Rasilimali na utajiri wa nchi unatumika hadi tone la mwisho bila kuwasaidia wananchi mahalia. Katika mantiki hii, Baba Mtakatifu anasikitika kusema, hata watu wanatumiwa kama vyombo vya kuzalishia mali na baadaye, wanatelekezwa pembeni, kama “daladala” iliyokatika usukani!

Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo unaofumbatwa katika kazi za suluba, biashara ya ngono ni mambo yanayowatajirisha watu wachache wenye uchu wa fedha na mali, kiasi cha kunyanyasa utu na heshima ya binadamu na kwamba, waathirika wakuu ni watoto na wanawake. Baba Mtakatifu amekemea pia tabia ya “mfumo dume” unaotembeza mkong’oto kwa wanawake na watoto majumbani, kiasi hata cha kushindwa kutambua dhamana, nafasi na mchango wa wanawake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu na heshima ya watoto wadogo hauthaminiwi. Matokeo yake ni vijana wa kizazi kipya kuikimbia nchi yao, ili kutafuta kesho iliyo bora zaidi kwa ajili yao na familia zao. Hawa ni vijana waliokimbia maisha ya unyenyevu na umaskini, lakini yaliyokuwa yanalinda na kuhifadhi utu wao kama binadamu. Matokeo yake wameambulia patupu, ile dhahabu waliyoona inang’aa, imegeuka kuwa ni chupa! Na vijana wameendelea kulipa gharama kubwa ya sadaka na maamuzi yao.

Uchu wa mali, fedha na madaraka vimewapelekea baadhi ya watu kudhani kwamba, wakiwa na mambo yote haya, wanaweza kununua kila kitu! Matokeo yake ni saratani ya rushwa kupamba moto, uharibifu wa misitu na udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu amewataka wananchi wa Puerto Maldonado kushinda kishawishi hiki kwa njia ya sala na kufunga; kwa kujenga na kudumisha Jumuiya ya Kikristo inayomzunguka Kristo Yesu. Kwa njia ya sala angavu na kweli; kwa watu kukutana ili kushirikishana Injili ya matumaini, wanaweza kuonja toba na wongofu wa ndani na hatimaye, kugundua maisha adili na matakatifu yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na wala si uchu wa fedha, mali na madaraka yanayowatumbukiza watu katika kifo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wokovu unamwambata mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, Jumuiya za Kikristo hazina budi kuzingatia utu wa watu, historia na sura zao, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kifamilia na kijumuiya, kama ushuhuda wa uwepo wa Ufalme wa Mungu, unaowashirikisha wote pasi na ubaguzi, kwani kila mtu anaitwa kwa jina, ili kuwa ni chombo cha kudumisha maisha kwa ajili ya wengine. Injili ya matumaini, iwawezeshe wananchi wa Perù kupenda na kuendelea kushangaa matendo makuu ya Mungu kwa ajili ya nchi yao, changamoto na mwaliko wa kuilinda, kuitunza na kuiendeleza, kama hazina itakayowawezesha kukua na hatimaye, kuwarithisha watoto wao, utajiri huu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.