2018-01-19 17:00:00

Papa: Ukoloni mamboleo unatishia usalama, maisha na ustawi wa Amazonia


Baba Mtakatifu Francisko ameianza siku ya pili ya hija yake ya kitume nchini Perù, Ijumaa tarehe 19 Januari 2018, kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Ubalozi wa Vatican nchini Perù na baadaye kuelekea mjini Puerto Maldonado, kiini cha msitu mkubwa wa Amazonia ambako amekutana na wawakilishi wa watu mahalia kwenye Uwanja wa michezo wa “Coliseo Madre de Dios” uliozinduliwa kunako mwaka 2013. Baba Mtakatifu amesikiliza shuhuda zilizotolewa na wenyeji na baadaye, akawakabidhi Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” uliotafsiriwa katika lugha mahalia.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amewashukuru wananchi wa Amazonia wanaoshuhudia utajiri wa kibayolojia, kitamaduni, maisha ya kiroho na hekima itakayowawezesha watu wengi zaidi kusimama kidete, kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwani hapa ni mahali patakatifu, ambapo panawawezesha watu kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani! Baba Mtakatifu anasema, yuko kati yao ili kuwatembelea, kuwasikiliza na kukaa pamoja nao ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, tayari kusimama kidete kulinda, kudumisha Injili ya uhai, mazingira na tamaduni.

Uwepo wa wananchi wa Amazonia kuliko wakati mwingine wowote katika historia yao, sasa wanatishiwa zaidi na nguvu za kiuchumi: zinazotafuta kuchimba mafuta, gesi asilia na madini; ni sera na mikakati ya kilimo cha mashamba makubwa kwa ajili ya kukidhi hitaji la malighafi ya viwanda pamoja na sera zisizotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kiasi kwamba,  watu wananyanyaswa na kudhulumiwa; rasilimali na utajiri uliopo ndani ya misitu hii hauwasaidii sana wenyeji na matokeo yake, vijana wa kizazi kipya wanakimbia ili kutafuta maisha bora zaidi ugenini. Umefika wakati wa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi wa Amazonia badala ya utajiri wa eneo hili kuyanufaisha mataifa tajiri. Ili kuweza kufikia sera na mikakati ya maendeleo endelevu kuna haja kwa taasisi kuwaheshimu na kuwathamini wananchi mahalia; kwa kujenga na kudumisha majadiliano na watu mahalia sanjari na kuzingatia: tamaduni, lugha, mapokeo, haki na amana ya maisha ya kiroho. Wananchi mahalia washirikishwe kwenye majadiliano yanayogusa kwa karibu zaidi maisha yao, ili kuondokana na tabia ya ubaguzi pamoja na wananchi mahalia kutengwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna “cheche za matumaini” zinazozijengea uwezo Jumuiya mahalia ili kusimama kidete kulinda na kutunza misitu na faida ya mazao yake, inawanufaisha wananchi mahalia kwa kuboresha hali ya maisha yao, huduma za afya na elimu.

Hii ni njia bora zaidi ya kuishi na kutenda; ni kilio cha watu mahalia, kinachopaswa kusikilizwa; kwa kutekeleza dhamana na wito ambao Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu, yaani kutunza mazingira nyumba ya wote kwani hatimaye yake ni kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, anafahamu mateso na mahangaiko yao yanayotokana na uchafuzi wa mazingira; uchimbaji haramu wa madini; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na nyanyaso za kijinsia; mateso na nyanyaso za wanawake na watoto majumbani. Hawa ni watu ambao utu na heshima yao viko mashakani kama alivyokuwa anasema Mtakatifu Turibius wakati wa maadhimisho ya Mtaguso III wa Lima, miaka mia tano iliyopita, lakini hata leo hii, kilio chao bado kinasikika. Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana yake ya kinabii kwa kuwa ni sauti ya wanyonge na wale wanaoteseka.

Baba Mtakatifu anasikitishwa sana na hali ya “wananchi mahalia ambao wametengwa kwa hiyari yao wenyewe” ( PIAV). Hawa ni watu ambao hawana tena uhuru, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana ili kuwatetea ili kuondokana na uwezekano wa kutokea kwa maafa makubwa kwa watu sanjari na uharibifu wa mazingira! Mwanadamu akumbuke kwamba, amepewa dhamana ya kulinda na kutunza mazingira na  Mwenyezi Mungu na wala si mmiliki wa kazi ya uumbaji. Kumbe, mtindo wa maisha na hekima ya watu mahalia iwasaidie watu wa Mataifa kujizatiti katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Amazonia.

Eneo la Amazonia ni alama ya maisha, hifadhi ya tamaduni na tofauti za kibayolojia; mambo ambayo yanapaswa kulindwa dhidi ya ukoloni mamboleo. Familia za watu mahalia daima zimekuwa mstari wa mbele kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, lakini kutokana na mwingiliano wa watu tamaduni hizi zinaanza kufifia, changamoto ni kusimama kidete kutunza tamaduni, mapokeo na lugha ili kuenzi hekima ya wahenga. Elimu inawasaidia watu kujenga daraja na utamaduni wa watu kukutana, kumbe hii inapaswa kuwa ni dhamana nyeti ya Serikali inayopaswa kutamadunishwa na kushirikishwa kama ustawi na mafao ya wananchi wengi. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa pia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu pamoja na kuwaendeleza watu mahalia. Vijana wafundwe vyema uelewa mpya wa binadamu, kusoma tena historia ya watu na maendeleo yao. Baba Mtakatifu anawashukuru wasanii wote kwa juhudi zao za kuonesha mwono wa ulimwemgu, utajiri wa tamaduni. Umefika wakati kwa wananchi mahalia kuandika historia ya nchi yao; kujitambulisha, kwani watu hawa wanahitaji kusikilizwa.

Amewapongeza wamissionari wanaojisadaka kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa Amazonia, dhamana ambayo wameitekeleza kama ushuhuda kwa Injili. Kristo Yesu alijilimwilisha katika tamaduni ya Kiyahudi, chachu mpya ya utambulisho wa mtu. Utamadunisho ni mchakato unaolitajirisha Kanisa na kwamba, Kanisa linataka kuwajengea uwezo wa kupambana na changamoto za maisha, ili siku moja Kanisa liweze kuwa na sura ya Amazonia inayofumbatwa na uwepo wa watu mahalia. Hiki ndicho kiini cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia itakayoadhimishwa mjini Vatican kunako mwaka 2019. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wataendelea kuimarisha mafungamano ya kijamii, kimaumbile na mang’amuzi ya imani. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, kwamba, anawaombea na kuwataka hata wao kumsindikiza kwa sala na sadaka zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.