2018-01-19 15:16:00

Papa Francisko tayari "ametinga timu" nchini Perù kwa kishindo!


Baba Mtakatifu Francisko na msafara wake wakati wa kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Chile, walipata chakula cha mchana kwenye nyumba ya mafungo ya “Nuestra Senora de Lourdes” yaani “Nyumba ya Bikira Maria wa Lourdes. Tukio hili limehudhuriwa pia na wagonjwa 10 pamoja na Bwana Hèctor Marin Rossel, mwakilishi wa waathirika wa vitendo vya dhuluma vilivyoikumba Chile kwenye miaka 1970 na baadaye, amemkabidhi barua Baba Mtakatifu Francisko. Bwana Hèctor Marin Rossel amemwelezea Baba Mtakatifu matumaini ya kuendelea kuwatafuta watu waliotekwa nyara na kupotea katika mazingira ya kutatanisha, kazi wanayoifanya kwa kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama nchini Chile. Amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kujisadaka kwa ajili ya kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu!

Baba Mtakatifu amewashukuru wote walioshiriki kuandaa chakula hiki na baadaye wakaondoka kuelekea kwenye Uwanja wa Ndege wa “Diego Aracena wa Iquique tayari kuondoka Chile na kuanza kuelekea Jimbo kuu la Lima, nchini Perù. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu amemtumia ujumbe wa matashi mema Rais Michelle Bachelet wa Chile. Amemshukuru kwa mapokezi makubwa na ukarimu ulioneshwa na wananchi wa Chile. Amewatakia wote heri na baraka pamoja na kuwahakikishia sala zake kwa ajili ya amani, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Chile. Baba Mtakatifu Francisko alipowasili Lima, nchini Perù amelakiwa na viongozi wa Kanisa na Serikali, chini ya uongozi wa Rais Pedro Pablo Kuczynski. Nyimbo za mataifa haya mawili zimerindima na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akakagua gwaride la heshima na baadaye akaelekea kwenye Makao makuu ya Ubalozi wa Vatican nchini Perù.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.