2018-01-19 15:36:00

Papa Francisko ni shuhuda wa Injili ya furaha kati ya watu wa Mungu!


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù kuanzia tarehe 18 - 22 Januari 2018 inaongozwa na kauli mbiu “Umoja wa Matumaini”. Kardinali Juan Luis Ciprian, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lima, nchini Perù anasema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao ni chachu kwa familia ya Mungu kumwendea na kumkaribia Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, chachu ya Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu anatembelea mji wa: Puerto Maldonado, alama ya watu wa Amazzonia, changamoto ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Papa Francisko atatembelea pia mji wa Trujillo ulioko Kaskazini mwa Perù, mji ambao uliathirika sana na mvua za El Nino, unaohitaji kukarabatiwa upya na mji wa Lima, madhabahu ya watakatifu wa Amerika ya Kusini.

Rais Pedro Pablo Kuczynski wa Perù katika tamko lake la kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini Perù anasema, licha ya tofauti zao msingi, lakini wana kiu ya kutaka kujenga na kudumisha nchi ambayo inafumbatwa katika msingi wa mshikamano bila ghasia. Perù ni nchi ambayo imejikita katika ushuhuda wa ukarimu unaofumbatwa katika maisha ya wananchi wake. Ni mahali ambapo dini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake.

Kardinali Juan Luis Ciprian anasema, Perù ni chemchemi ya maisha ya watakatifu wengi kutoka Amerika ya Kusini. Ni mahali walipozaliwa akina Rose wa Lima, Mtakatifu Martin de Porres pamoja na Mtakatifu Francesco Solano. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanajikita katika mchakato wa utamadunisho wa Injili, ili kupyaisha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kutambua dhamana na wajibu wao wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji! Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa utume wa Uinjilishaji. Baba Mtakatifu Francisko yuko kati yao kama mjumbe wa umoja wa matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.