2018-01-18 15:42:00

Papa Francisko anawashukuru wote waliojisadaka kwa ajili ya hija yake


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwaombea wananchi wa Chile kwenye Uwanja wa Lobito, Jimbo Katoliki la Iquique na kabla ya kuondoka kuelekea PerĂ¹, Alhamisi tarehe 18 Januari 2018 amewashukuru viongozi wa Kanisa na Serikali na wale wote waliojisadaka usiku na mchana ili kufanikisha hija hii ya kitume nchini Chile. Kwa namna ya pekee, amemshukuru Rais Michelle Bachelet wa Chile aliyemwalika kutembelea nchini mwake. Baba Mtakatifu anasema, bila juhudi za watu mbali mbali walioshirikiana kwa karibu muujiza wa divai ya furaha usingewezekana.

Amewashukuru wale wote waliomsindikiza kwa njia ya sala na sadaka zao, ili kufanikisha utamaduni wa watu kukutana na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, sasa anakaza macho yake kuelekea nchini PerĂ¹, watu ambao ni ndugu na marafiki wa karibu wa wananchi wa Chile, mwaliko ni kusaidiana kwa hali na mali. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia imani na umoja anapohitimisha hija yake ya kitume nchini Chile. Anawaomba kuendelea kusali na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.