2018-01-18 08:36:00

Papa: Dhamana ya Chuo Kikuu ni kufundisha, kufikiri na kutenda


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Chile na kuwataka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kutambua kwamba, wao ni kiini cha mageuzi ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, alitembele Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Chile, Jumatano, tarehe 17 Januari 2018. Hiki ni Chuo Kikuu ambacho kwa takribani miaka 130 kimetoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu nchini Chile. Hapa pamekuwa ni mahali pa majiundo ya awali na endelevu kwa mamilioni ya wananchi wa Chile.

Kanisa lina mkumbuka kwa namna ya pekee, Mtakatifu Alberto Hurtado, ambaye miaka mia moja iliyopita alianza masomo yake Chuoni hapo. Maisha yake ni ushuhuda unaoweka uwiano mzuri kati ya akili, uwezo wa masomo darasani na weledi katika kutekeleza dhamana na majukumu yanayomwilishwa katika misingi ya imani, haki na upendo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mambo yote haya yanapata nguvu za kinabii, zinazomwezesha mwamini kuwa na mwelekeo mpana zaidi na mwanga wa kuona na kuwahudumia wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Changamoto kubwa kwa familia ya Mungu nchini Chile kwa wakati huu ni “umoja wa kitaifa na maendeleo ya jumuiya”. Ili kukuza na kudumisha umoja wa kitaifa kuna haja ya kutazama upya mambo yanayoifungamanisha jamii zaidi na kuyapatia majibu muafaka pasi na haraka. Chuo kikuu kinapaswa kuwa ni mahali pa kukuza na kudumisha mchakato wa mabadiliko unaofumbatwa katika majadiliano yanayojenga utamaduni wa watu kukutana. Ikumbukwe kwamba, hekima ya kweli anasema Baba Mtakatifu ni tafakari, majadiliano na mkutano kati ya watu. Mshikamano wa kitaifa ni jambo linalowezekana, kwa kukazia zaidi mfumo wa elimu unaopaswa kuwa ni chachu ya maendeleo kwa kuzingatia tunu msingi za elimu zinazotolewa kwenye Chuo Kikuu: kwa kufundisha, kufikiri na kutenda kama sehemu ya mchakato endelevu. Haya ndiyo majiundo ya akili “forma mentis”. Ili kuweza kufikia hatua hii ya maendeleo endelevu ya binadamu kuna haja ya kushirikisha lugha mbali mbali zinazowatambulisha kama watu; elimu inayoweka uwiano mzuri kati ya: akili, moyo na matendo; mambo msingi yanayoweza kuwasaidia wanafunzi kukua na kukomaa kama mtu binafsi na kama jamii. Elimu iwasaidie wanafunzi: kufikiri na kutekeleza kile wanachofikiri kama sehemu muhimu sana ya huduma kwa binadamu na jamii katika ujumla wake. Mchakato wa elimu uwawezeshe wanafunzi kushirikishwa zaidi katika masuala ya elimu ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza huko mbeleni.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mawazo hayana budi kumwilishwa katika lugha, ili kuwaunganisha watu. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni watu kufikri na kutenda katika ombwe bila ya kuwa na msingi thabiti na matokeo yake, maisha ya hadhara hayana nafasi tena na hivyo ubinafsi kushika kasi ya ajabu. Maisha ya kijumuiya yapewe msukumo wa pekee zaidi, ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa. Watu wawe na utambuzi wa kumbu kumbu zinazowatambulisha kama: familia, jamii na taifa! Bila umoja na mshikamano, watoto hawana matumaini ya kesho iliyo bora zaidi na kwamba, ubinafsi utaota mizizi na matokeo yake ni kinzani na mipasuko ya kijamii. Kutokana na changamoto hizi, Chuo kikuu hakina budi kuhakikisha kwamba, kinatoa mwelekeo sahihi ili kujenga mshikamano na ukuaji wa jumuiya. Kumbe, Chuo kikuu cha Kikatoliki kinapaswa kuwa pia ni mahali pa uinjilishaji, chemchemi ya furaha  ya Injili inayolipyaisha Kanisa, tayari kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Jumuiya ya Chuo Kikuu itambue kwamba, ina dhamana na wajibu wa kimissionari kwani huko wanakutana na watu mbali mbali.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Chuo Kikuu lazima kijikite katika tafiti ili kutoa mwelekeo sahihi utakaojenga na kuimarisha dhana ya Jumuiya inayofundisha, ili kukabiliana na changamoto mamboleo kwa kuwa na ufahamu mpana zaidi; kwa kuzingatia mambo msingi ya maisha ya wananchi wa Chile, ili kuweka uwiano mzuri kati ya kile kinachofikiriwa na kusikika; kile kinachofahamika na kile ambacho watu wanakiishi kwa ajili ya huduma ya Injili ya uhai ili kupata maendeleo endelevu na shirikishi kwa watu wote. Ufahamu hauna budi kuwa na mwingiliano kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa “Jumuiya ya Waborijene” kwa kuzingatia tamaduni na mapokeo yao, ili hata wao waweze kujisikia kuwa wadau katika mchakato wa maendeleo yanayogusa maisha yao kwa karibu zaidi!

Jumuiya inayofundisha inabeba utajiri mkubwa wa watu wake, wanaoshirikishana tunu msingi, lakini jambo la kuzingatia ni kuhakikisha kwamba,  kuna ubora na ushirikishwaji wa watu, ili kweli Chuo kikuu kiweze kuwa ni maabara ya ustawi na maendeleo ya nchi kwa kuvuka vikwazo vya kinzani na mipasuko ya kijamii. Sayansi isipopewa kipaumbele cha pekee, majanga yatamwandama mwanadamu, lakini pia mwanadamu anapaswa kukumbuka kwamba, ameumbwa na Mwenyezi Mungu na anapaswa katika maisha yake, kutafuta kile kilicho haki, chema, kizuri na cha kweli! Majaalimu wa vyuo vikuu, wawe wagunduzi ili kuwasaidia wanafunzi wao kugundua ulimwengu, tayari kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kinabii. Chuo kikuu kiwe ni chachu ya mabadiliko na mageuzi ya ubinadamu uliopyaishwa; kwa kujikita katika majadiliano ili kuepuka kinzani na mipasuko ya kijamii; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni matumaini yake kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Chile, kitaendelea kuzaa matunda bora kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Chile na kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Na Padre Richard A, Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.