2018-01-17 11:06:00

Petro mtume aliyeanguka, akasamehewa na kutakaswa awe mfano wa Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Chile, mara baada ya kutembelea na kuzungumza na wafungwa wa kike wanaotumikia adhabu yao kwenye Gereza kuu la Wanawake la Santiago linalojulikana kama “Gereza la “San Joaquin”, Jumanne, jioni, tarehe 16 Januari 2018 alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi kutoka Chile. Katika tafakari yake, alimchambua kwa namna ya pekee, Mtakatifu Petro aliyebwagwa chini kutokana na udhaifu wake wa kibinadamu; Petro Mtume, aliyesamehewa na Petro mtume aliyetakaswa na kuwa mtu mpya kabisa, kiasi cha kudhaminishwa na Kristo Yesu, kuwachunga na kuwalinda Kondoo wake!

Baba Mtakatifu alianza tafakari yake kwa kuwakumbusha wakleri na watawa umuhimu wa kupyaisha “Ndiyo” yao kila kukicha, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Katika safari ya maisha, wito na utume wao, wakumbuke kwamba, kuna nyakati za kuteleza na kuanguka kama mtu binafsi au jumuiya; kuna nyakati za kutubu na kuonja msamaha na hatimaye, kuna muda wa kutakaswa na kuundwa upya. Haya ni mambo changamani na kamwe hayawezi kutenganishwa. Wito na utume wa kipadre na kitawa ni picha inayopaswa kupigwa na mtu mwingine tofauti ili kutambua uzuri na mapungufu yako!

Baba Mtakatifu anasema, Injili daima imejikita katika ukweli na uwazi, kwa kuonesha nyakati ambazo Mitume wa Yesu wamezipitia katika maisha yao, kiasi hata cha kuteleza na kuanguka kama ilivyotokea kwa Mtakatifu Petro. Baada ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Mitume walihitaji muda wa kuweza kutafakari na kung’amua kile kilichotendeka na utimilifu wa mang’amuzi haya ni Siku kuu ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume na kuwapatia ari na mwamko mpya wa kusonga mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kabla ya Pentekoste, Mitume, walianza kurejea tena katika maisha yao ya zamani, wakarudi kuvua samaki ambako hata huko nako wakaambulia patupu! Mitume walikabiliana na upweke hasi na hali ya kukata tamaa baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu. Mtakatifu Petro, anakumbuka wazi kwamba, alimkana Yesu mara tatu, Yuda Iskarioti alikwisha “kwapua” vipande thelathini vya fedha na wengine, “walichanja mbuga na kutokomea mahali kusiko julikana” kwani hapa kulikuwa ni patashika nguo kuchanika anasema Baba Mtakatifu. Hiki ni kipindi cha giza katika maisha ya Mitume wa Yesu, hali ambayo iliwapelekea kuona mateso, dhuluma na mashaka kuhusu maamuzi ya maisha yao.

Katika kipindi kama hiki, anasema Baba Mtakatifu, kishawishi kikuu ni kutaka kupembua mawazo bila kuyapatia uzito unaostahili, kukita mawazo kwa wanaowadhulumu na mbaya zaidi ni kujitumbukiza katika hali ya kujikatia tamaa ya maisha. Hii ndiyo hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa nchini Chile kama ilivyopembuliwa na Kardinali Ricardo Ezzati Andrello, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santiago katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na wakleri pamoja na watawa! Kanisa limepitia changamoto pevu katika maisha na utume wake; limeonesha uaminifu na udumifu lakini hata hivyo, magugu ya dhambi na udhaifu wa binadamu yameendelea kukua ndani ya Kanisa na matokeo yake ni kashfa na maasi yanayoshuhudiwa hata leo hii nchini Chile.

Kashfa za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zina madhara makubwa katika maisha na utume wa Kanisa; kwa waathirika pamoja na familia zao, hali inaoibua hofu na mashaka, kiasi cha kutoliamini tena Kanisa na matokeo yake Kanisa limetikisika sana. Hapa kuna haja ya kusema ukweli na uwazi, kwa kuwa na ujasiri wa kuitaja dhambi hii kwa jina bila kumung’unya maneno, ili kufanya toba na hatimaye, kuomba msamaha. Jamii ya Chile inakumbana na mabadiliko ya haraka katika tamaduni, mwingiliano wa watu, matamanio ya “masufuria ya nyama huko Misri” na kusahau kwamba, leo na kesho iliyo bora zaidi iko miguuni pa wananchi wenyewe! Mabadiliko kama haya yanaweza kuwatumbukiza wananchi wa Chile kujifungia katika ubinafsi wao na kudhani kwamba, yote ni ubatili mtupu! Changamoto mbele ya Kanisa ni kusimama tena kifua mbele na kuanza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuziangalia changamoto zote hizi kwa macho makavu, tayari kuonesha ujasiri wa kumfuasa Kristo hata katika shida na magumu ya maisha. Kuna baadhi ya Mitume walikuwa tayari kutumia upanga kwa ajili ya kumlinda Yesu, wakathubutu kuomba mvua ya moto, ili iwaoneshe cha mtema kuni waliokataa kumkaribisha Yesu.

Baba Mtakatifu anasema hatua ya pili inamwonesha Petro Mtume, aliyesamehewa, kwa kutambua ukweli wa maisha yake; ambao hakutaka hata mara moja kuuangalia usoni, akajiaminisha kupita kiasi na kusahau udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, kiasi hata cha kumkatisha tamaa Yesu aliyekua amemteua kuwa mwamba wa Kanisa lake. Hii ni hali inayoweza kuwakumba wafuasi wa Kristo na Kanisa katika ujumla wake kwa kushindwa kuona udhaifu wake na badala yake kujificha katika umaarufu! Yesu alimuuliza Petro mara tatu, ikiwa kama alikuwa anampenda kwa dhati, ili kumwokoa kutoka katika ubinafsi na upweke wake; hofu na machungu moyoni, ili aweze kung’amua ukweli unaofumbatwa katika upendo! Petro mtume, anaungama wazi wazi kwamba, Yesu mwenyewe anafahamu undani wa maisha yake na anaomba huruma ya Yesu, ili iweze kumwambata tena!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni changamoto ya kutambua kwamba, kama Wakristo ni watu ambao wamesamehewa na hiki ndicho kiini cha furaha ya maisha na utume wao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Mapadre na watawa wanapaswa kuwaendea watu kwa heshima na nidhamu, kwa kuguswa na Madonda Matakatifu ya Yesu, yanayojionesha kati ya watu, ili kuyaganga na kuyaponya. Kwa madonda na mapungufu ya Kanisa, Kristo anakuwa ni kiini cha maisha na utume wake, ili aweze kuwaokoa na kupyaisha tena maisha yao; kwa kubomoa kuta za utengano na kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana. Mapadre na watawa wanapaswa kuwa ni watu wenye kujisadaka, wanaothubutu kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa kupambana na hali na mazingira ya maisha yao ya kila siku, tayari kugusa uhalisia wa maisha ya watu wao; kwa kufungua macho, ili kutolea sala na sadaka mahangaiko ya watu, mbele ya Mwenyezi Mungu. Familia ya Mungu inahitaji mapadre na watawa ambao ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama ilivyokuwa kwa Kristo mwenyewe!

Hatua ya tatu anasema Baba Mtakatifu ni pale ambapo Kristo Yesu alipomtakasa Petro, akimkumbusha kwamba, ukuu ndani ya Kanisa ni huduma, kama alivyofanya yeye mwenyewe kwa kuwaosha miguu mitume wake, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake! Jambo la msingi ni unyenyekevu, ari na moyo mkuu, tayari kuwahudumia watu wa Mungu waliojeruhiwa katika maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro. Kanisa halina budi kujielekeza katika Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi; kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; daima likisimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili watu wote waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu. Toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa.

Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kutambua udhaifu wao, tayari kutubu na kujipyaisha tena katika huruma na upendo wa Mungu unaomwokoa mwamini, daima wakiwa tayari kurejea tena kuchota upya wa maisha kutoka katika Injili tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni, anawataka wakleri na watawa kumwachia nafasi Kristo Yesu, ili aweze kuwapyaisha, kwa njia ya ushuhuda unaofumbatwa katika utakatifu wa maisha na utume wa Kanisa; kwa kutambua na kuguswa na mahangaiko ya maskini, tayari kuwatangazia Injili ya huduma ya upendo. Kanisa lililojeruhiwa lipate faraja na uponywaji wake kutoka katika Madonda Mtakatifu ya Kristo Yesu, tayari kwa wakleri na watawa kurudia tena ile “Ndiyo” yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.