2018-01-16 15:49:00

Papa: Heri wapatanishi na wenye kiu ya haki, wataitwa wana wa Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia na viongozi wa vyama vya kiraia, Jumanne, tarehe 16 Januari 2018 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa O’Higgins – Santiago, Jimbo kuu la Santiago na kuhudhuria na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya  Chile. Katika Ibada hii, Liturujia ya Neno la Mungu imejikita katika “Heri za Mlimani”, Upatanisho na Mungu kama msingi wa upatanisho wa kijamii, amani na utulivu.  Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee kuhusu “Heri za Mlimani” muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu.

Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mwanaye wa Pekee, Kristo Yesu anatamani sana kukutana na waja wake ili aweze kuwaangalia usoni na kuwaonjesha huruma na upendo wake wa daima! Yesu katika maisha na utume wake alikutana na watu, akasikiliza kilio chao na kuwaonjesha maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Heri za Mlimani ni changamoto inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kwani zinabubujika kutoka kwenye Kisima cha huruma ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Unaotambua mahangaiko ya binadamu na watu wanaojibidisha kutafuta heri; watu wanaoteseka na kumezwa na majanga ya maisha kama “ndoto ya mchana” lakini hata hivyo bado wanatoka kifua mbele kusonga mbele kwa kuanza upya!

Huu ndio mfumo wa maisha ya wananchi wa Chile wenye uwezo wa kusimama tena baada ya kuanguka, kwani ndani mwao wanao msingi wa “Heri za Mlimani”. “Heri za Mlimani ni kanuni inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kama sehemu ya mchakato wa mabadiliko na ujenzi wa jumuiya na maisha mapya! Heri za Mlimani zinapata chimbuko lake kutoka katika Moyo wa huruma unaosimikwa katika matumaini. Yesu anakazia kuhusu maskini, wanaohuzunika, wanaoteseka na kusamehe, wote hawa wanaonjeshwa furaha dumifu na endelevu badala ya kukimbia matatizo, kujificha kutoka kwa wengine kwa kujifungia katika ubinafsi na ulaji wa kupindukia. Hii ni hali ya kukata tamaa inayowatenganisha waamini na watu wengine na kushindwa kuona tena maana ya maisha na mahangaiko ya wengine!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Heri za Mlimani” ni mapambazuko ya siku mpya, inayojikita katika matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi yanayobubujika kutoka katika roho ya Mungu. Yesu kama jua la haki anakuja kuwashirikisha roho ya Mungu wale wote wanaojizatiti kwa mwanzo wa siku mpya, yaani Chile mpya kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wao, kwani wapatanishi na wenye kiu ya haki wataitwa wana wa Mungu. Kamwe wananchi wasikate tamaa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho, ili kujenga amani na umoja wa kitaifa, chemchemi ya furaha ya kweli! Wale wote wanao tamani amani, wanapaswa kujizatiti kuitafuta amani na kumwilisha katika haki inayozingatia utu na heshima ya binadamu.

Kupandikiza amani ni nguvu ya ujenzi wa udugu miongoni mwa wananchi wote wa Chile; kwa kufutulia mbali chuki na uhasama; uchu wa mali na madaraka; kwa kutafuta umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko! Amani ya kweli inamwilishwa katika matendo mema kama anavyokazia Mtakatifu Albert Hurtardo. Mchakato wa ujenzi wa amani unahamasisha na kuunganisha kipaji cha ubunifu ili kujenga mafungamano ya kijamii yanayofumbatwa katika uzalendo, umoja na udugu wa wananchi wa Chile. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wananchi wote wa Chile chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili awasaidie kutamani “Heri za Mlimani” ili wote waweze kuwa wajenzi wa amani kwani wamekuwa ni watoto wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.