2018-01-16 08:30:00

Papa Francisko asikitishwa sana na madhara ya vita duniani!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea Chile kwenye hija yake ya kitume ya ishirini na mbili kimataifa, Jumatatu, tarehe 15 Januari 2018 alipata nafasi ya “kuchonga” pamoja na waandishi wa habari ambao wako kwenye msafara wake huko Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kukazia rufuku ya kutengeneza, kutumia na kulimbikiza silaha za kinyuklia kwani madhara yake ni makubwa sana katika maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Inatosha ajali kidogo tu! na Jumuiya ya Kimataifa ikajikuta inakabiliwa na janga kubwa!

Baba Mtakatifu ameyasema haya baada ya kugawa picha ya mtoto kutoka Nagasaki,  Japan ambaye mgongoni mwake, alikuwa amebeba maiti ya mdogo wake aliyeuwawa kikatili wakati wa mashambulizi ya mabomu ya atomic huko Nagasaki, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kunako mwaka 1945. Chini ya picha hii iliyopigwa na Joseph Roger O’Donnell kutoka nchini Marekani, ameandika kwa msisitizo, “Haya ndiyo matokeo ya vita”. Picha ya mtoto huyu inaonesha jinsi ambavyo alivyokata tamaa, kiasi hata cha kutafuna midomo yake iliyokuwa inabubujika kwa damu! Alikuwa amejipanga kwenye mstari, akisubiri zamu ya mazishi ya mdogo wake! Picha hii inagusa na kuchoma dhamiri za watu kuliko hata litania ya maneno!

Baba Mtakatifu anasema, vita haina macho wala pazia, wanaoteseka na maskini na wanyonge zaidi, kumbe kuna haja ya kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa amani duniani! Amewapongeza waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake kwa kuwaambia kwamba, mbele yao kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuweza kuwajuza watu wa mataifa kile kinachoendelea huko Amerika ya Kusini. Anasema, anaifahamu Chile vyema zaidi, kwani katika maisha yake, alipata nafasi ya kusoma nchini humo kwa muda wa mwaka mmoja! Safari hii imedumu kwa takribani muda wa masaa 16.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.