2018-01-15 08:39:00

Hija ya Papa Francisko nchini Perù: Mapambazuko ya umoja wa kitaifa!


Askofu mkuu Salvador Pineiro Garcia-Calderon, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Perù, anapenda kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwapatia zawadi ya kuwatembelea kama sehemu ya hija yake ya kitume Amerika ya Kusini, inayoongozwa na kauli mbiu “Umoja wa matumaini”. Maandalizi ya kiroho na kimwili, imekuwa ni fursa iliyowashirikisha wananchi wengi kutoka ndani na nje ya Perù ili kuhakikisha kwamba, tukio hili linafanikiwa. Hija hii ni zawadi kubwa kwa familia ya Mungu nchini Perù inayotaka kujenga na kudumisha utamaduni wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Umoja unapata chimbuko lake katika familia na baadaye unamwilishwa katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Ni changamoto ya kung’oa ndago za chuki, uhasama na utengano unaodhohofisha mshikamano na mafungamano ya kijamii. Kanisa nchini Perù kama ilivyo kwa Amerika ya Kusini ni hai na tena lina nguvu inayofumbatwa katika umoja wa Wakleri, Watawa na Waamini walei katika ujumla wao! Huu ni mwanzo mpya wa Kanisa linalotaka kujenga na kudumisha utamaduni wa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hili ni Kanisa linalopania kuendeleza majadiliano katika ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi.

Askofu mkuu Salvador Pineiro Garcia-Calderon anaendelea kufafanua kwamba, umoja huu unajikita katika mambo matakatifu, ushuhuda makini wa watakatifu wanaoheshimiwa nchini Perù, lakini kwa namna ya pekee sana watakatifu kama Rosa wa Lima na Mtakatifu Martin de Porres: amana na utajiri mkubwa katika maisha ya kiroho na tunu msingi za Kiinjili. Hawa ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Hawa ni watakatifu waliolipamba Kanisa la Kristo kwa njia ya ushuhuda wa huduma makini kwa maskini pamoja na kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na kwamba, damu yao imekuwa ni mbegu nzuri ya Ukristo huko Amerika ya Kusini.

Askofu mkuu Salvador Pineiro Garcia-Calderon anasema, Kanisa linataka kuendeleza mchakato wa majadiliano na maridhiano ili kweli família ya Mungu nchini Perù iweze kushikamana, ili kujenga na kudumisha: umoja na udugu; haki, amani na uhuru wa kweli. Kumbe, familia ya Mungu nchini Perù inataka kumwonjesha Baba Mtakatifu Francisko cheche za furaha ya Injili katika maisha yao. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kujitokeza kwa wingi ili kushiriki kikamilifu katika matukio mbali mbali yatakayo adhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 19 Januari 2018 hadi tarehe 22 Januari 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.