2018-01-15 09:53:00

Familia ya Mungu nchini Chile inataka kujenga utamaduni wa amani!


Askofu Santiago Jaime Silva Retamales, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Chile anapenda kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko anapoanza hija yake ya kitume nchini Chile, Jumatatu tarehe 15 Januari 2018 kwa kumwomba aweze kujisikia kuwa nyumbani, licha ya changamoto mbali mbali atakazokabiliana nazo. Wamejiandaa kikamilifu ili kumpokea Baba Mtakatifu kati yao kama: Mchungaji mkuu wa Kanisa, Baba na ndugu atakayezungumza nao kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye ni mwamba ambao Kristo Yesu, amejenga Kanisa lake juu yake.

Hii ni nguvu ya kulinda na kutunza imani, maadili na utu wema; daima akijitahidi kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu kama kiongozi mkuu wa Kanisa la Kristo, tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Baba Mtakatifu anataka kuwaonesha moyo wa upendo na mshikamano wa dhati, hasa zaidi na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wote hawa waweze kufunuliwa na hatimaye, kuona huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Hii ni changamoto ya kusimama kidete, kulinda na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, uharibifu wa mazingira ni chanzo kikuu cha maafa kwa binadamu! Kila mwananchi anayo dhamana na wajibu wa kujenga na kudumisha ulimwengu bora zaidi unaofumbatwa katika: haki, upendo, umoja na udugu, ili kukuza na kuendeleza mchakato wa amani, maridhiano na mafungamano ya kijamii unaopania kujenga jamii iliyo bora zaidi. Kumbe, haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele na wote sanjari na kujikita katika majadiliano yanayofumbata ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi.

Miaka 30 iliyopita, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Chile na sasa familia ya Mungu iko tayari kusikiliza maneno ya Baba Mtakatifu Francisko. Roho Mtakatifu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ataiwezesha familia ya Mungu kujenga na kudumisha: amani, umoja, mshikamano na upendo. Familia ya Mungu nchini Chile inatambua fika umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa amani unaojikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; amani inayojenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii na kwamba, amani ni tunda la haki inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Chile. Baba Mtakatifu Francisko anataka kukazia zawadi ya amani na utulivu miongoni mwa familia ya Mungu nchini Chile, ili kufungua ukurasa mpya wa upatanisho wa kitaifa, maridhiano na umoja wa kitaifa kama asemavyo Mzaburi: fadhili na kweli zimekutana, haki na amani zimebusiana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.