2018-01-14 14:37:00

Wakimbizi na wahamiaji wapamba Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuziacha nchi zao na kwa wale wanaoishi katika hali na mazingira magumu! Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuhudhuriwa na wawakilishi wa wahamiaji na wakimbizi kutoka katika nchi 49 ambao walibeba bendera za nchi zao.

Kumekuwepo pia na idadi kubwa ya mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa mjini Vatican waliohudhuria Ibada hii. Wakristo kutoka madhehebu mbali mbali walipewa tiketi za kuweza kuhudhuria na kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, ambayo pia imepambwa kwa nyimbo kutoka katika lugha mbali mbali, lakini kwaya kuu ilikuwa ni kwaya ya “Hope” kutoka Jimbo kuu la Torino, Italia. Takwimu zinaonesha kwamba, Liturujia hii, imehudhuriwa na wamissionari wengi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika hutoaji wa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia.

Waamini wamesali na kuliombea Kanisa ili liweze kuwa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote na kwamba, wajisikie kupendwa, kupokelewa na kukombolewa. Waamini wajitahidi kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa na kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wawe waaminifu kumfuasa Mwana Kondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Kanisa limewakumbuka na kuwaombea watu wote wanaoishi katika umaskini pamoja na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha, ili waweze kuonja huruma na faraja kutoka kwa jirani zao. Kanisa limewaombea watu wote wanaoteseka, wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaongoa watu hawa. Waamini wanaoshiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu wapate amani na utulivu wa ndani. Mwishoni, Kanisa limewaombea wakimbizi na wahamiaji wote waliofariki dunia, wapate maisha ya uzima wa milele na hatimaye, waweze kuuona uso wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.