2018-01-10 11:44:00

Kwa msaada wa Roho Mtakatifu, Liturujia iwe ni shule ya sala!


Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Huu ni utangulizi wa Neno la Mungu kwenye Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatofu Francisko, Jumatano, tarehe 10 Januari 2018. Huu ni mwendelezo wa Katekesi kuu maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Tendo la toba linawawezesha waamini kujiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu na kujiona jinsi walivyo; kwa kujitambua kwamba, ni wadhambi, lakini wenye matumaini ya kuweza kusamehewa dhambi zao!

Baba Mtakatifu anasema, huruma ya Mungu inamwilishwa kwa namna ya pekee katika Wimbo wa Utukufu kwa Mungu Juu, wimbo wa zamani sana ambamo Mama Kanisa anayekusanywa chini ya Roho Mtakatifu, anamtukuza na kumwomba Mwenyezi Mungu na Mwana Kondoo! Huu ni wimbo unaopata chimbuko lake kutoka kwa Malaika wakati wa kuzaliwa kwa Kristo Yesu mjini Bethlehemu. Hii ni mbiu ya furaha juu mbinguni na duniani, inayowaunganisha waamini wanaosali “Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema”. Baada ya Wimbo wa Utukufu na kama haupo, mara tu baada ya “Tendo la Toba”, kunafuatia “Sala fupi” inayofafanua maana ya adhimisho la siku hiyo, mintarafu siku na kipindi cha Mwaka. Na kwa mwaliko wa “Tuombe”, Padre mhudumu, anawaalika waamini kukaa kimya kwa kitambo, ili kutambua kwamba, wako mbele ya Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko kwa kila mwamini kuzama katika undani wa moyo wake, kuunganisha nia ambazo amekuja nazo kushirikisha wakati wa Ibada ya Misa Takatifu.

Hapa Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa ukimya, ili kuweza kusikiliza sauti ya ndani kabisa inayotoka kwa Roho Mtakatifu. Katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu inategemea kwa kiasi kikubwa kipindi kinachofuatia kwani, waamini wanahamasishwa kusali baada ya Mahubiri kama ilivyo pia mara baada ya Kupokea Ekaristi Takatifu. Lengo ni kuwasaidia waamini kusali kutoka katika undani wa maisha yao. Kumbe, ukimya katika Ibada ya Misa Takatifu ni muhimu sana, ili kumwezesha mwamini kutambua kwamba, yeye ni nani, ili kusikiliza nyoyo na kuifungua kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Pengine, waamini wanaodhuhuria Ibada hii ya Misa Takatifu ni wale wanaopambana na magumu katika maisha; ni watu wanaobubujika furaha, au wana majonzi; yote haya waamini wanataka kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumwomba aweze kuwa karibu na waja wake. Huu ni muda wa sala kwa ajili ya ndugu, jamaa na marafiki wagonjwa au wanaoteseka kutoka na majaribu makubwa ya maisha. Kumbe, waamini wanataka kumtolea Mwenyezi Mungu matumaini ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anawataka mapadre kutokuwa na haraka wakati wa "Sala ya Tuombe", watoe muda wa ukimya muhimu sana  kwa waamini kuweza kujikusanya tena kutoka katika undani wao. Katika mazingira kama haya, Mapadre wanaadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu wakiwa wamefungua mikono yao, kielelezo cha mwamini anayesali. Ni ushuhuda unaoneshwa pia katika ”Mapango ya Kale” kama yanavyojulikana kama ”Macatacombe ya Kiroma”, ili kumuiga Kristo Yesu aliyefungua mikono yake pale Msalabani. Ni Kristo anayesali, Kwa njia ya Kristo Mteswa, waamini wanamtambua Padre anayetoa sadaka kwa Mwenyezi Mungu kama kielelezo cha shukrani na utii wa kimwana.

Katika Liturujia ya Kiroma Sala ya Maombi ina utajiri mkubwa, changamoto na mwaliko kwa waamini kufanya tafakari ya kina kwenye sehemu hizi za sala, ili kujifunza namna ya kumwomba Mwenyezi Mungu sanjari na kuchagua maneno ya kutumia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kwa msaada wa Roho Mtakatifu Liturujia itaweza kuwa kweli ni shule ya sala. Hii inatokana na ukweli kwamba, Ibada ya Misa Takatifu ina utajiri mkubwa wa sala za kijumuiya pamoja na nafasi kwa sala binafsi. Hapa waamini wanaweza kujifunza namna ya kusali vyema. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawatakia wote neema na baraka, ili kweli kipindi cha Mwaka Mpya wa 2018 kiwe ni kipindi cha neema, amani na matumaini. Bikira Maria awe ni shuhuda wa imani na matumaini kati ya ndugu, jirani na marafiki zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.