2018-01-06 10:16:00

Siku ya Utoto Mtakatifu Duniani: Jengeeni watoto moyo wa kimissionari


Katika Sherehe ya Tokeo la Bwana inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimissionari ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, njaa, ujinga na umaskini. Hata katika umaskini wao, watoto wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia!

Hii ni changamoto inayotolewa na Sr. Roberta Tremarelli, Katibu mkuu wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, katika maadhimisho ya Siku ya Utoto Mtakatifu sanjari na Sherehe ya Tokeo la Bwana. Hii ni siku maalum iliyoanzishwa na Papa Pius XI, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee katika maisha na utume wake. Watoto wanapaswa kujifunza na kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni!

Mshikamano wa upendo, umewawezesha watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuguswa na mahangaiko ya watoto wenzao kiasi cha kujinyima na kuchangia kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao! Sr. Roberta Tremarelli anasikitika kusema, leo hii, haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia zinaendelea kuvunjwa, kiasi kwamba, watoto wananyanyaswa na kudhulumiwa; wanapokwa haki yao ya utoto kwa kufanyishwa kazi za suluba; kwa kusumbuliwa na: umaskini, magonjwa, ujinga, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; kwa vita na majanga mbali mbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu!

Watoto hata katika changamoto zote hizi, bado wanaweza kusaidiwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari, kwa kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano. Kwa njia hii watoto wamesaidia kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuwapatia watoto wenzao mahitaji msingi kama vile: chakula, elimu, makazi na huduma bora ya afya. Shirika la Utoto Mtakatifu lililoanzishwa kunako mwaka 1843 na Askofu Toussaint de Forbin Janson wa Jimbo Katoliki la Nancy. Mwaka huu wa 2018, Shirika la Utoto Mtakatifu linaadhimisha Jubilei ya Miaka 175 tangu kuanzishwa kwake. Taarifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2016 jumla ya miradi 2, 621 imefadhiliwa sehemu mbali mbali za dunia kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 15. 6.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.