2018-01-06 12:13:00

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Watu walimtafuta, hawakumjali, wakamwogopa


Mwinjili Mathayo katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anakazia mambo makuu matatu: Mamajusi kutoka mashariki waliothubutu kumtafuta Mtoto Yesu, Mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa mjini Bethlehemu kwa kuongozwa na nyota; tabia ya kutojali iliyooneshwa na wakuu wa makuhani na waandishi ya wa watu, waliofahamu fika Maandiko Matakatifu kiasi cha kuonesha mahali alipozaliwa Masiha, lakini wao, hawakujitaabisha kuifuata nyota hiyo!

Kundi la tatu ni Mfalme Herode aliyegubikwa na hofu kubwa sanjari na kufadhaika na Yerusalemu pamoja naye. Alihofia kwamba, Mtoto Yesu aliyezaliwa angempora Ufalme wake. Ndiyo maana alimtafuta Mtoto Yesu kwa "udi na uvumba" si kwa ajili ya kumwabudu, bali kwa kutaka kumfutilia mbali kwa upanga kwani alionekana kuwa ni mpinzani wake nambari moja! Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Tokeo la Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 6 Januari 2018.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ubinafsi unaweza kuwatumbukiza watu kudhani kwamba, ujio wa Kristo Yesu unahatarisha uwepo wao na matokeo yake ni kuanza kutafuta njia za kutaka kunyamazisha Habari Njema ya Wokovu. Haya ni matokeo ya watu kumezwa sana na malimwengu; kwa kutafuta raha, faraja na anasa, kiasi cha kumwona Yesu kuwa ni hatari katika kutekeleza matamanio yao ya kibinadamu! Kwa upande mwingine, kuna kishawishi cha kutojali, hata kama waamini wanafahamu fika kwamba, Kristo Yesu ni Mkombozi wa ulimwengu lakini wanashindwa kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake na matokeo yake ni watu kumezwa na malimwengu na kutumbukia katika uchu wa mali na madaraka.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumtafuta Kristo Yesu kwa "udi na uvumba" katika maisha yao, ili hatimaye, waweze kukutana naye katika maisha. Lengo ni kumwabudu kwa kutambua kwamba, Kristo ni Bwana, Njia, Ukweli na Uzima na kwamba, ni Mkombozi wa dunia, mambo ambayo yatawawezesha waamini kuishi maisha mazuri, kukua katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka waamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Nyota ya binadamu anayefanya hija katika nyakati, ili kwa njia ya maombezi yake, watu wote waweze kumfikia Kristo Yesu: Mwanga wa ukweli na hivyo kuwawezesha walimwengu kujikita katika ukuzaji wa misingi ya haki na amani duniani.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka Wakristo wa Makanisa ya Mashariki wanaodhimisha Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2018. Maadhimisho haya ni chemchemi ya maisha mpya ya kiroho na umoja miongoni mwa Wakristo wote wanaomtambua na kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi. Sherehe ya Tokeo la Bwana ni Siku ya Utoto Mtakatifu, mwaliko kwa watoto kumtazama Mtoto Yesu, ili aweze kuwaongoza katika utume wao wa: sala, udugu, ushirikiano na mshikamano na watoto wenzao ambao ni wahitaji zaidi. Mwishoni, amewasalimia waamini na mahujaji wote kutoka ndani na nje ya Italia na kwa namna ya pekee, wasanii waliongoza maandamano ya Sherehe ya Tokeo la Bwana kuzunguka viunga vya mji wa Vatican, kama walivyofanya Mamajusi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.