2018-01-05 06:45:00

Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa, Mfalme na Mkombozi wa Ulimwengu


Leo tunaadhimisha sherehe ya Epifania. Ni sherehe inayohitimisha kipindi cha Noeli, kipindi cha kuzaliwa mkombozi wetu Yesu Kristo. Katika sherehe ya leo tunaadhimisha Tokeo la Bwana, na ndiyo maana ya Epifania, yaani Kristo kujifunua au kujitambulisha kwa mataifa. Habari za kuzaliwa kwa Kristo zilisambaa ndani ya uyahudi kuanzia kwa wachungaji waliopashwa habari na malaika. Tukio la leo linaashiria kusambaa kwa habari hizi nje ya mipaka ya uyahudi. Injili ya leo inatuonesha namna Mamajusi watatu kutoka nchi za mashariki walivyoongozwa na nyota kuja Bethlehemu kumsujudia Kristo aliyezaliwa. Wakampa kama zawadi dhahabu, uvumba na manemane zawadi ambazo zinabeba maana katika maisha yake.

Kristo anajifunua kuwa ndiye mwanga wa mataifa aliyekuja kuiangazia Yerusalemu, kuiamsha na kuirejeshea utukufu wake. Yeye ndiye mwanga ambao mataifa watatembea kwa njia yake. Huu ndio ujumbe wa unabii wa Nabii Isaya tunaousikia katika somo la kwanza, ujumbe unaokamilika kwa kuzaliwa kwake Kristo. Kwa sherehe hii ya leo Kristo anapojitambulisha kwa mataifa anatupatia ujumbe kuwa hakuja kwa ajili ya wayahudi pekee bali amekuja kwa ajili ya watu wote. Amekuja ili wote wauone mwanga, waufuate na wakombolewe kwa njia yake. Katika tafakari ya leo tutajikita kuuangalia ujio wa Kristo kama ujio wa mwanga na chachu mpya ya maisha ya mwanadamu.

Kuzaliwa kwa Kristo kulisubiriwa kwa hamu kubwa sana. Tangu anguko la Adamu na Eva ulimwengu ulibaki katika hali ya kupungukiwa kitu muhimu katika uwepo wake. Ulibaki katika hali hiyo ukisubiri kwa hamu kukombolewa kutoka hali hiyo. Katika injili tumesikia kuwa nyota ilipowafikisha mamajusi mahali alipozaliwa Yesu “walifurahi furaha kubwa mno”. Mwinjili anaielezea furaha hiyo kuwa ilikuwa ni ya kiwango cha juu. Haikuwa tu furaha, bali ilikuwa furaha kubwa, na hakuishia hapo akaongeza ilikuwa furaha kubwa mno! Hii ni furaha ambayo mtu huwa nayo pale anapopata kitu cha thamani kubwa  alichokuwa amepoteza au alichokuwa anasubiri. Mamajusi hawa kutoka nchi za mashariki wanauwakilisha ulimwengu uliokuwa ukimsubiri Kristo masiha na wanaiwakilisha furaha yake kubwa mno iliyoipata baada ya kuzaliwa kwa Kristo masiha. Kwa nini ulimwengu ulimsubiri Kristo kwa hamu kubwa hivyo?

Kwanza ni kwa sababu ulimwengu mzima ulikuwa na giza na haikuwezekana kuona mbele. Mwanadamu ambaye aliumbwa ili aishi milele na Mungu mbinguni alifukuzwa bustanini Edeni baada ya dhambi kuingia ulimwenguni. Na kisha kufukuzwa, mbingu ilifungwa. Tangu wakati huo mwanadamu aliishi bila kuona hatima ya maisha yake iliyokusudiwa na Mungu, hakuona mbele na aliishi katika giza kwa sababu asingeweza tena kuiona nuru ya uso wa Mungu. Nuru hii inaletwa na Kristo pekee. Ni nuru hii Kristo aliifikisha ukamilifu wake pale alipojitoa sadaka na kufa msalabani kama fidia ya dhambi za mwanadamu. Zawadi ya manemane aliyopewa na mamajusi ni zawadi inayoashiria kifo chake ili kuudhihirisha mwanga kwa mwanadamu na kwa ulimwengu mzima.

Pili ulimwengu ulimsubiri Kristo kwa sababu  haukuwa na mwelekeo. Mtume Paulo katika waraka wake kwa Wakolosai anatuambia kuwa Kristo ndiye kichwa cha viumbe vyote. Katika yeye vyote viliumbwa... yeye ndiye mtangulizi katika yote na katika yeye upo utimilifu wote (rej. Kol. 1:13-20). Kama kundi linavyohangaika likikosa kiongozi na kama mwili usivyo kamili bila kichwa ndivyo ulivyokuwa ulimwengu bila mwanga wa Kristo.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatuambia kuwa Mamajusi hawa walifika Bethlehem  kumsujudia mfalme wa wayahudi ambaye ndiye mfalme wa mataifa yote (KKK. 528). Mataifa yalimuhitaji Kristo mfalme kwa sababu wafalme waliokuwa nao hawakuwa na uwezo wa kuwatimizia mahitaji yao halisi. Hiki ndicho inachoashiria zawadi ya dhahabu ambayo mamajusi walimpatia Yesu. Injili imetupatia mfano wa mfalme Herode kuonesha aina ya ufalme na uongozi katika mataifa uliojaa hila, ukatili, uuaji na unaokosa hofu ya Mungu. Ni ufalme unatotaka kuuzima mwanga wa Kristo na unaoona uwepo wa Kristo ni tishio kwake. Ndivyo alivyofanya kwa kwa kuwadanganya mamajusi kuwa naye anahitaji kumsujudia mtoto Yesu lakini kwa hakika alihitaji kumuua.

Tatu ulimwengu ulimsubiri Kristo kwa sababu ulihitaji kupatanishwa na Mungu na ni Kristo pekee ambaye angeuleta upatanisho huu. Mwanadamu aliyejitenga na Mungu kwa sababu ya dhambi zake asingeweza kujipatanisha mwenyewe, wala si kwa Torati wala si sadaka za kuteketezwa walizozitoa. Torati iliwakusanya pamoja kama wana wa agano na sadaka za kuteketezwa zilikuwa ni hitaji la kiibada lisiloweza kuwaondolea hatia ya dhambi ya asili. Mtume Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa Timoteo anatuambia “mpatanishi kati ya wanadamu ni mmoja Kristo Yesu, ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote (1Tim. 2:5-6). Naye Kristo ndiye Kuhani mkuu wa Agano Jipya na la milele. Na tena ni kuhani, altare na mwanakondoo kwa maana ndiye aliyejitoa sadaka kwa ajili ya upatanisho wetu. Na zaidi ya hayo akaweka sakramenti ya upatanisho ili mwanadamu aendelee kusafishwa na kila doa la dhambi. Ukuhani huu wa Kristo unaashiriwa na zawadi ya uvumba waliyomtolea mamajusi.

Ujumbe huu wa sherehe ya leo ni ujumbe unaotualika kuufurahia uwepo wa Kristo katika ulimwengu na katika maisha yetu.  Tuuone uwepo wake kuwa umekuja kuubadilisha ulimwengu, kuupa mwanga, kuupa mwelekeo na kutupatanisha sisi wenyewe na Mungu muumba wetu. Uwepo wa Kristo umekuja kuumba upya ulimwengu. Ni katika mantiki hii tunaona kuwa jitihada zozote za kuufifisha uwepo wa Kristo katika maisha yetu na katika ulimwengu ni kujirudisha katika giza ambako hatutapata mwelekeo wa maisha na hatimaye tutajitenga kabisa na Mungu. Yeye mwenyewe anasema  Mimi ndimi nuru ya ulimwengu; yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima" (Yohana 8:12).

Tukingali mwanzoni mwa Mwaka huu Mpya 2018 tuombe neema ya kubaki katika mwanga wa Kristo. Kuongoza maisha yetu katika mwanga huo ili tufikie uzima aliotufaidia kwa kuzaliwa kwake duniani. Bikira Maria mama wa Msaada wa daima atuombee.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre William Bahitwa

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.