2018-01-04 12:03:00

Ratiba elekezi kwa Papa Francisko kufunga kipindi cha Noeli 2018


Ratiba elekezi iliyotolewa mjini Vatican inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 5 Januari 2018 Majira ya Alasiri, anatarajiwa kutembelea Hospitali ya Watoto ya “Bambino Gesù” inayomilikuwa na kuendeshwa na Vatican kama chombo cha ushuhuda makini kwa huduma ya watoto! Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kutembelea watoto wagonjwa pamoja na wazazi wao wanaowatunza hospitalini hapo! Ni nafasi ya kutoa salam na matashi mema kwa wafanyakazi wanaojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya huduma makini kwa watoto wagonjwa pamoja na familia zao! Watoto wana upendeleo wa pekee katika utume wa Papa Francisko!

Jumamosi, tarehe 6 Januari 2018, majira ya Saa 4: 00 Asubuhi Sherehe ya Tokeo ya Bwana, maarufu kama Epifania, Siku kuu ya Mwanga, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni Siku pia ya Shirika la Utoto Mtakatifu linalojikita katika malezi ya watoto wadogo ili kuwajengea ari na mwamko wa kimissionari, tayari kuwainjilisha watoto wenzao kwa njia ya utume wa sala na huduma makini, hususan miongoni mwa watoto maskini na ambao hawakubahatika kuwa na maisha bora kama watoto wengine.

Siku hii pia waamini wanahamasishwa kuchangia kwa hali na mali katika kukuza na kudumisha mchakato wa uinjilishaji hasa katika nchi za kimissionari duniani, ili kujenga Ufalme wa Mungu duniani, ufalme unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano. Hizi ni juhudi za Mama Paulina Jaricot aliyependa kuona Kanisa linawajengea watoto ari na mwamko wa kimissionari kwa kujali, kusikiliza na kujibu kilio cha watoto wenye shida kutoka sehemu mbali mbali za dunia!

Jumapili, tarehe 7 Januari 2018 majira ya saa 3: 30 Asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, inayofunga shamra shamra zote za kipindi cha Noeli. Katika Ibada hii itakayoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Sistina, Papa Francisko anatarajiwa kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto walioandaliwa, ili waweze kuzaliwa upya kwa “Maji na Roho Mtakatifu” tayari kushiriki: ukuhani, ufalme na unabii wa Kristo Yesu. Baadaye mchana ataongoza Sala ya Malaika wa Bwana.

Jumatatu, tarehe 8 Januari 2018, majira ya Saa 4:30 Asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko atakutana na kusalimiana na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi, mashirika na taasisi mbali mbali za kimataifa mjini Vatican. Ni nafasi ya kutakiana salam na matashi mema, mwanzoni kabisa mwa mwaka 2018. Vatican News, itaendelea kukushirikisha yale yanayojiri katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.