2018-01-03 15:35:00

Papa Francisko: Dhambi inamtenganisha mwamini na Mungu na jirani


Tuendelee na katekesi yetu kuhusu maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kufikiria leo hii katika mantiki za liturujia ya utangulizi kwa tendo la kuungama. Kwa uwazi wake inasaidia kwa maana ni tendo la kujiweka tayari ili kustahili kuadhimisha mafumbo matakatifu na kutambua dhambi zetu mbele ya Mungu na ndugu zetu. Mwaliko wa Kuhani kwa kawaida unawalenga waamni wote katika sala kwasababu wote tu wadhambi. Je Bwana anaweza kuzawadia nini yule ambaye moyo wake tayari umejaa ubinafsi na mafanikio yake binafsi? Hakuna, kwasababu anayejidai hana uwezo wa kupokea zawadi hiyo kwa maana ,amejazwa haki ya majivuno yake.

Ni maneno ya utangulizi wa tafakari ya  Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake siku ya tarehe 3 Januari 2018 katika Ukumbi wa Mwenye heri Paulo VI mjini Vatican. Baba Mtakatifu Franciko ameanza Katekesi hii mwa mwaka mpya ikiwa ni mwendelezo wa Mada ya Maadhimisho ya Misa, akitafakari kipengele cha  tendo la maungamo kabla ya kuanza misa. Tafakari lake limeanza mara baada ya kusoma somo kutoka katika Barua ya kwanza ya Mtakatifu Paulo isemayo: Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe kile cha baraka tukibarikicho,je!Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.

Akifafanua zaidi juu ya maungamo, Baba Mtakatifu anasema tufikirie katika Injili juu ya  maelezo ya Mfarisayo na mtoza ushuru, mahali ambapo mtu wa pili alirudi nyumbani akiwa na haki yake, kwa maana ya kusemehewa dhambi zake (Lk 18,9-14). Hiyo ni kutokana na kwamba, mwenye utambuzi wa udhaifu wake na kuinamisha macho yake kwa unyenyekevu, anahisi kupokea ndani yake mtazamo wa huruma ya Mungu. Tunatambua kwa uzoefu  ya kuwa,  kwa yule anayetambua makosa yake na kuomba msamaha anapokelewa na kusamehewa na wengine.

Baba Mtakatifu anaongeza: Kusikiliza kwa ukimya sauti ya dhamiri nafsi , inasaidia kutambua kuwa mawazo yetu kweli yako mbali na mawazo ya Mungu, na maneno na matendo yetu  ambayo daima yamebobea  na kiulimwengu kutokana na kuongozwa daima na  uchaguzi binafsi, ni tofauti na ya Injili. Kwa njia hiyo wakati wa kuanza Misa, tunafanya tendo la  pamoja la kutubu kwa sala maalumu ya kuungama. Kila mmoja anaungama kwa Mungu na kwa ndugu kutokana na  dhambi nyingi za mawazo, maneno, matendo na kutotimiza wajibu, Baba Mtakatifu anasisitiza kuwa, ndiyo, hata kutotimiza wajibu, kwa maana ya kuacha kutenda wema ambao unatakiwa kuutenda.

Daima tunahisi kuwa wema na kusema “ mimi sijamtendea mtu baya”. Lakini kiukweli haitoshi kutomtendea jirani vibaya, kwani inatakiwa kuchagua kutenda yaliyo mema kwa ajili yake, kutumia fursa mbalimbali ili kutoa ushuhuda mwema ya kwamba, sisi ni wafuasi wa Yesu. Kwa maana hiyo, kusisitiza katika maungamano kwa Mungu na ndugu kuwa tu wadhambi, inasaidia kutambua ukubwa wa dhambi ambazo zinatutengenisha na Mungu, kututenganisha na ndugu zetu na mengineyo. Baba Mtakatifu amesisitiza , dhambi inakatisha mahusiano na Mungu, inakatisha mahusiano na ndugu, familia, jamii na jumuiya kwa ujumla,dhambi daima inakata mahusiano na inatengenisha!

Maneno lakini tunayotamka kwa mdomo yanasindikizwa na ishara ya kujipiga kifuani, kwa utambuzi wa dhambi zetu tulizo nazo, lakini si kwa mwingine,Baba Mtakatifu anasisitiza. Hata hivyo anabainisha kwamba. wakati mwingine tunayo tabia ya kuogop au aibu, tunadiriki  kunyoshea  wengine mikono na kuwahukumu. Kwa maana inagharimu kujihukumu dhambi binafsi,lakini ni vema kwetu sisi kuungama kwa dhati na kuungama dhambi binafsi.

Hapa Baba Mtakatifu ametoa mfano akisimulia kisa kimoja ya kuwa, mmisionari mzee aliwasimulia historia ya mwanamke mmoja aliyekwenda kuungama,akaanza kusema makosa ya mme  wake; baadaye makosa ya mkwewe, baadaye dhambi za jirani zake. Lakini mara moja  muungamishi baada ya kumsikiliza akamwambia je mama,umemaliza?, akajibu  hapana”....Muungamishi akaendelea ni vizuri;  basi sasa umemaliza kuungama dhambi za wengine  sasa anza kusema dhambi zako binafsi….! Baba Mtakatifu Francisko akiwa na maana ya kwamba kuungama maana yake ni kuungama dhambi binafsi na siyo dhambi za mwingine!

Akiendelea na ufafanuzi anasema, baada ya sala ya maungamano, tunaomba Bikira Maria mwenye heri, Malaika na Watakatifu wote kutuombea kwa Bwana. Anabainisha, hata maombezi hayo ni yenye thamani kubwa ya umoja wa watakatifu: Ni maombezi ya hawa marafiki na mfano wa kuigwa wa maisha, ambao wanatusimamia katika safari kuelekea katika ukamilifu wa umoja na Mungu, wakati ule wa mwisho, dhambi zitakapokuwa zimeangamizwa kabisa.

Pamoja na hayo katika  maungamo unaweza kufanya  tendo la kutubu kwa njia ya sala nyingine kwa mfano  Bwana utuhurumie/ kwakuwa tu wadhambi./ Tuoneshe huruma yako Bwana, Tupatie wokovu wako (Taz Zab 123,3;85,8; Yer 14,20) na zaidi siku ya Jumapili, inawezekana kufanya tendo la baraka kwa kunyunyizia maji, kama ishara ya kumbukumbu ya Ubatizo. Inawezaka kama sehemu ya tendo la kuungama, kuimba wimbo wa Kyrie eléison: Kielelezo cha kizamani cha Kigiriki, kwa kutamka Bwana (Kyrios) na kuomba huruma yake.

Maandishi matakatifu yanatoa  fursa ya mifano wazi ya sura za waungama kweli, ambao mara baada ya kujitafiti dhamiri zao binfsi kwa kutenda dhambi walipata ujasiri wa kuondoa vitambaa machoni,na kujifungua katika neema ambayo inaunda upya moyo. Baba Mtakatifu anabainisha watu hao kwamba, tufikirie Daudi na maneno yake aliyoandika katika Zaburi ya 51; Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. 

Fikirieni mwana mpotevu ambaye anarudi kwa Baba yake; au maombi ya mtoza ushuru:ee Mungu unionee huruma mimi mwenye dhambi (Lk 18,13). Tufikirie Mtakatifu Petro na Zakayo na mwanamke msamaria. Kujipima udhaifu kama udongo wa mfinyanzi ambao tumetengenezwa kutoka kwake, ni uzoefu ambao unatuimarisha, kwa maana tunapokuwa na utambuzi wa udhaifu wetu, tunafunguka moyo na kuomba huruma ya Mungu ambayo inageuza na kutoa uongofu. Baba Mtakatifu amemalizia kwa kusema hilo ndilo tendo tunalofanya wakati wa sala ya kutubu katika utangulizi wa Misa!

Sr Angela Rwezaula
Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.